Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewataka wakazi wa Dunda ‘A’ na Dunda ‘B’ wajiunge
kwenye Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na wavisajili kwenye Halmashauri yao ili
waweze kukubalika kupatiwa mikopo. Alikuwa akizungumza na wakazi wa eneo hilo Jumanne,
Januari 28, 2014, lililopo Mtaa wa Kigogo Fresh Kata ya Pugu wilaya ya Ilala nje kidogo
ya Jiji la Dar es Salaam kwenye hafla fupi ya uzunduzi wa kisima cha maji kwa ajili
ya wakazi wa eneo hilo.
Waziri Mkuu aliwataka wasajili vyama vyao ili waweze
kutambulika kwa urahisi na waweze kuwa na watu wenye dhamana ya kurejesha mikopo mara
watakapoanza shughuli za ujasiriamali. “Tatizo letu ni ukosefu wa anuani za makazi
ili wakopaji watambulike na waweze kurejesha mikopo. Tunasisitiza SACCOS kwa sababu
tunajua kutakuwa na watu wenye dhamana ya kusimamia urejeshwaji wa mikopo hii,” alisema
wakati akijibu swali la Bw. Abdallah Mwaking’inda na wakazi wa Dunda.
Vilevile,
alitumia fursa hiyo kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick
afuatilie shule ambazo zinatoza michango kwa watoto waliopaswa kuandikishwa darasa
la kwanza lakini wakashindwa kuazna shule kwa sababu ya michango hiyo. “Uandikishwaji
wa watoto wanaoanza darasa la kwanza ni wa lazima kwa kila mtoto, tulifanya hivyo
ili tuhakikishe watoto wote wapate elimu. Sasa kama mzazi ana watoto wawili au watatu
akishindwa kuwalipia manake watoto hao wamebaki nyumbani,” alisema.
“RC litazame
vizuri suala hili kwa sababu kama zoezi la uandikishaji ni hili, ina maana kuna wazazi
watashindwa kuwapeleka watoto shule,” alisema.
Mapema, kwenye risala yao, wakazi
hao wa Dunda ‘B’ walimshukuru Waziri Mkuu kwa kuwaunganisha na mfadhili kutoka taasisi
ya REHEMA ambayo imewajengea kisima hicho chenye urefu wa mita 90, tenki la lita 10,000
na mnara wa mita 20 wa kuwekea tenki hilo kwa gharama ya sh. milioni 20. Walimwomba
pia Waziri Mkuu awasaidie kupata umeme wa three phase ili uweze kutosheleza mahitaji
ya eneo zima la Dunda ikiwa ni pamoja na kuendesha kisima chao.
Akijibu haoja
hiyo, Mhandisi Theodori Bayona kutoka TANESCO makao makuu alisema watarudisha huduma
ya three phase iliyokuwepo zamani lakini ikaondolewa kwa sababu ya wizi wa mara kwa
mara. Aliwaomba wakazi hao wawe walinzi wa nyaya pindi watakapowekewa na kwamba watatakiwa
kulipia service line ya kawaida ili umeme upelekwe hadi kisimani moja kwa moja.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick aliwahidi kuwachangia tenki moja
la lita 10,000 ili waweze kuwa na ujazo mkubwa wa maji kwenye matenki yao na kuepusha
kazi ya kupampu maji mara kwa mara. Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, wenye magari
yanayobeba maji, wanauza ndoo moja kwa sh. 400/- katika eneo hilo.