2014-01-29 09:15:47

Altare ni kielelezo cha Kristo anayejisadaka! Mzungukeni wakati wa shida na raha!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Dominika III ya Mwaka (26 Januari 2014), ametabaruku Altare ya Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Petro, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Kanisa la Parokia hii lilizinduliwa mwaka 1958, na Altare yake ya asili ilijengwa wakati ambapo Padri alikuwa anatazama ukuta. Mabadiliko ya mwadhimishaji kuwatazama waamini yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, yalitekelezeka kwa shida, kwani kulikuwa na nafasi finyu kati ya ukuta na Altare.

Hali hii iliwasukuma waamini na viongozi wa Parokia, kwa kushauriana na Mchungaji Mkuu wa Jimbo, kujenga Altare mpya. Altare hii ni ya jiwe tupu, ambalo limechongwa na Watawa wa Mt. Benedikti wa Abasia ya Ndanda, Jimbo Katoliki la Mtwara.

Waamini wa parokia ya Mtakatifu Petro, dominika iliyotangulia siku ya kutabarukiwa kwa Altare, walipata katekesi juu ya maana ya altare na ya kutabarukiwa. Juu ya maana ya altare, waamini walikumbushwa kwamba, Altare iliyo hai ni Kristo mwenyewe. Hivyo wanavyoiona Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka msalabani. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Kristo, wanapaswa kutambua kuwa wao ni sehemu ya Altare. Ndiyo maana kila mmoja anapaswa kuwa sadaka, kwa Mungu na kwa jirani. Aidha, chochote kinachotabarukia kinapaswa kutumika kwa ajili ya Mungu tu, kama vile kila mbatizwa anavyopaswa kuwa kwa ajili ya Mungu, kinyume chake ni kujiteketeza.

Kardinali Pengo katika mahubiri yake alisisitiza juu ya upekee wa altare katika maisha ya kila siku. Altare ni Kristo katika hali yake yote. Ni Kristo mzima, anayewaponya, kufundisha; anayeteswa, aliyekufa na kufufuka. Altare ni meza ya karamu, hivyo waamini wanapokuwa na furaha, wakusanyike Altareni. Vivyo hivyo Altare ni Msalaba ambapo Kristo alijitoa sadaka, hivyo wanapokuwa na huzuni na mahangaiko mbalimbali, waizunguke Altare. Kwa kuwa Altare ni Kristo mzima, wamfuate wakiwa katika hali yoyote wanayoweza kuwa nayo, Yeye yupo siku zote katikati yao anawangoja, katika magumu na furaha.

Katika tukio hili la kutabaruku Altare, pia alishiriki Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Ghalib M. Bilal, ambaye anaishi karibu na Kanisa hili, alikaribishwa kama jirani wa Parokia, pamoja na Rais Mstaafu Benjamini Mkapa. Makamu wa Rais alipata nafasi ya kutoa nasaha zake, na alisisitiza umuhimu wa umoja na upendo miongoni mwa Watanzania. Tunu hizi mbili ndizo waasisi wa Taifa la Tanzania wamewachia kama ulirithi wao, hivyo wanapaswa kuzitunza kwa gharama yoyote ile.

Mwisho wa ibada, waamini walifanya harambee ya kuchangia ukamilishwaji wa ukumbi wa Parokia. Pesa taslimu pamoja na ahadi zilifikia milioni themanini, pamoja na ahadi ya vifaa mbalimbali vya ujenzi. Makamu wa Rais kama ishara ya mshikamano alichangia milioni kumi.








All the contents on this site are copyrighted ©.