Upembuzi yakinifu wa Mapapa katika matumizi ya vyombo vya upashanaji habari!
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya njia za mawasiliano ya jamii yamewawezesha viongozi
wa Kanisa kuufikia umati mkubwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Matumizi ya vyombo
vya upashanaji habari imekuwa ni changamoto kwa Mama Kanisa katika Uinjilishaji mpya
katika mapambazuko ya millenia ya tatu. Ni changamoto iliyovaliwa njuga kwa namna
ya pekee kabisa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ikaendelezwa na Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI na kwa sasa Papa Francisko anaonekana kushika usukani katika
njia ya za mawasiliano ya jamii ndani na nje ya Vatican.
Ni tafakari iliyotolewa
na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican na mkurugenzi wa Radio Vatican,
Jumatatu tarehe 27 Januari 2014, wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 20
tangu ilipozinduliwa Radio Maria Toledo na Kituo cha Televisheni cha Jimbo vilipoanzishwa.
Katika maadhimisho haya Padre Federico Lombardi amepewa tuzo ya heshima kwa kutambua
mchango wake mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu katika masuala
ya vyombo vya upashanaji habari.
Padre Lombardi anasema kwamba, changamoto
ya matumizi makini ya vyombo vya habari iliyotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo II
ilifanyiwa kazi na majimbo mbali mbali dunia kwa kuanzisha vituo vya Radio na Televisheni.
Padre Lombardi anakumbuka baadhi ya matukio ambayo watu walitamani kumwona Baba Mtakatifu
akishiriki katika mateso na mahangaiko ya watu!
Baada ya shambulio la kigaidi
lililofanyika tarehe 11 Septemba huko Marekani, liliwashtua watu wengi wakajiona wanyonge
sana mbele ya macho ya magaidi. Katika hali kama hii, watu wengi walitamani kumwona
na kumsikia Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili akiwapa neno la faraja. Kituo cha Televisheni
cha Vatican kikamwonesha Papa akisali kwa ajili ya waathirika wa shambulio la kigaidi.
Watu
wengi bado wanakumbuka ile hija ya upatanisho na msamaha iliyofanywa na Baba Mtakatifu
Yohane Paulo II kwenye gereza ili kumtembelea na kuzungumza na Ali Agca, aliyemshambulia
kwa risasi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huu ulikuwa
ni ushuhuda wa Injili ya Huruma ya Mungu iliyomwilishwa katika matendo adili. Ni kwa
njia ya Televisheni hadi leo hii, ile picha ya Mwenyeheri Yohane Paulo II bado iko
mioyoni mwa watu!
Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa
ni mtu aliyefahamu kutumia vyema vyombo vya mawasiliano ya kijamii, kwa njia ya maneno
na vitendo vyake. Kwa njia ya televisheni watu wengi walishuhudia hija za kichungaji
zilizofanywa na Papa Yohane Paulo II sehemu mbali mbali za dunia. Wengi bado wanakumbuka
siku ile Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili aliposali na kutumbukiza ujumbe wake kwenye
ukuta wa Yerusalem, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.
Papa Yohane Paulo II alikwenda Yerusalem kuomba msamaha kwa dhambi zilizotendwa na
Watoto wa Kanisa.
Padre Lombardi anasema miaka 25 ya Utume na Maisha ya Baba
Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, yameacha kumbu kumbu za kudumu katika akili na miyo
ya watu. Hii ni kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya mawasiliano ya Jamii. Hata katika
unyonge na magonjwa yake, Kituo cha Televisheni cha Vatican kilimwonesha Papa Yohane
Paulo wa II kwa heshima na taadhima; watu wakaonja na kushiriki Njia ya Msalaba hadi
pale alipokata roho na kujikabidhisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma
na mapendo.
Papa Yohane Paulo II alipenda daima kufanya tafakari ya hija zake
za kichungaji na wasaidizi wake wa karibu ili kusikia mwangwi wa ujumbe wake na kuona
ikiwa kama kweli ujumbe aliokusudia kuutoa umewafikia wengi. Kwa maneno machache,
Papa Yohane Paulo II alikuwa ni rafiki wa vyombo vya habari.
Padre Federico
Lombardi ambaye kwa miaka saba ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI alikuwa naye bega kwa bega anasema, Papa aliendeleza uhusiano wake na vyombo vya
habari, lakini kwa bahati mbaya, uhusiano huu ulikuwa tenge. Mara kwa mara waandishi
wa habari walimtupia "madongo" Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Alijitahidi
kujenga uhusiano wa karibu na vyombo vya habari kadiri alivyoweza. Majibu kwa maswali
yaliyoulizwa na waandishi wa habari ni yale ambayo yalibubujika kutokana na tafakari
na maandalizi ya kina na hitimisho kwa ajili ya wasikilizaji wake.
Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto alianzisha mtindo wa kuzungumza na waandishi wa habari wakati wa
hija zake za kichungaji, ili kujadili kuhusu lengo na kiini cha hija zake za kichungaji.
Wakati mwingine majibu yake yaliyosheheni msimamo wa Kanisa kuhusu maadili na utu
wema yalizua kinzani na matusi kutoka kwa baadhi ya wanaharakati waliotumia vyombo
vya habari ili kumshambulia Papa mstaafu Benedikto XVI. Ni kurasa chungu, lakini zilipita
kwa amani na utulivu.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI atakumbukwa sana
na Mama Kanisa kwa kuliachia Kanisa urithi wa tafakari ya kina kuhusu maisha ya Yesu
wa Nazareti, akionesha umahiri wake katika tafakari ya Neno la Mungu, Taalimumungu,
Tasaufi, Katekesi na Mafundisho ya Kanisa. Watu bado wanakumbuka maneno na unabii
wa Papa Mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika mahojiano na Peter Seewald kuhusu:
Mwanga wa Ulimwengu".
Alijitahidi kujibu maswali hata yale yaliyokera katika
maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini bado aliendelea kuwa
ni kiongozi mwenye imani na matumaini. Hata hivi karibuni waandishi wa habari "walimtwanga"
swali Papa Francisko kuhusu "mashoga". Kumbe, si rahisi kuweza kuwaridhisha waandishi
wa Habari, kwani kila chombo kina mtazamo na malengo yake.
Kimsingi Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI ameacha urithi mkubwa kwa Kanisa katika maisha ya kiroho, Tafakari
ya Neno la Mungu, Katekesi, kwa kuzingatia ukweli na uwazi. Kuna mambo ambayo alikuwa
anaandika kwa mkono wake mwenyewe anasema Padre Lombardi. Katekesi zake alizokuwa
anatoa kila Jumatano zimekuwa ni msingi mkubwa wa Katekesi endelevu katika maisha
na utume wa Kanisa.
Makleri wa Jimbo kuu la Roma wanakumbuka ile Katekesi
ya kina kuhusu Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican aliyoitoa kwa muda wa
masaa matatu yote akiyachambua kutoka katika hazina ya moyo wake! Matendo makuu ya
Mungu! Siki tatu baadaye, akatangaza kung'atuka kutoka madarakani kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Ulimwengu ukapigwa na butwaa! Kwa hakika Papa Mstaafu
Benedikto XVI hakubahatika kuwa na umati mkubwa wa watu waliomfuata na kumsikiliza,
kama ilivyo kwa Papa Francisko, lakini waliobahatika kumsikiliza walibaki wakiwa wameshika
tama!
Padre Federico Lombardi anasema, Papa Francisko anaonekana kuwa na mvuto
pamoja na mashiko kwa vyombo vya habari hata vile ambavyo vilikuwa vinafuatilia maisha
na utume wa Kanisa kwa "makengeza" sasa wanaanza kubadili mwelekeo. Ni Kiongozi mwenye
mvuto kwa watu wengi; mnyenyekevu, mkweli na muwazi. Ni kiongozi anayeguswa na mahangaiko
ya watu na kuyafanyia kazi.
Ni kiongozi anayeendelea kuwashangaza wengi kwa
kuvunja kuta za utengano, ili kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikishana imani,
matumaini na mapendo. Ni kiongozi mwenye karama kubwa ya mawasiliano. Si mtaalam sana
wa lugha, lakini kile kidogo alichojaliwa na Mwenyezi Mungu anakitumia kikamilifu!
Papa Francisko ambaye hazungumzi Kiingereza hivi karibuni alichaguliwa na TIME MAGAZINE
kuwa ni mtu mashuhuri kwa Mwaka 2013.
Padre Lombardi anasema, Papa Francisko
pengine anaweza kuongoza kwa kupigwa picha na watu mbali mbali katika kipindi hiki
kifupi cha maisha na utume wake. Ni picha zinazoonesha uwepo wa karibu kwa wagonjwa,
maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; wote hawa anapenda kuwaonjesha:
upendo na huruma ya Mungu. Radio Vatican inatasiri ujumbe wa picha hizi katika lugha
40 zinatumika katika matangazo yake kila siku!
Papa Francisko analichangamotisha
Kanisa kupembua mbinu mkakati wa mawasiliano katika maisha na utume wake, kwa kuhakikisha
kwamba, linatumia vyombo vya mawasiliano ya Jamii kwa ajili ya kutangaza Injili ya
Furaha sanjari sanjari na utekelezaji wa mikakati ya kichungaji. Watu wanatamani kuona
kwamba, vyombo vya habari vinawasaidia kumwona, kumsikia na kumfuasa. Hapa kunaonekana
uhusiano wa dhati kati ya utume wa Baba Mtakatifu Francisko na dhamana ya vyombo vya
habari.
Ni matumaini ya Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kwamba,
vyombo vya habari kitaifa na kimataifa vitamsaidia Baba Mtakatifu Francisko kuwahudumia
watu wa mataifa, ili kuwaonjesha: huruma na upendo wa Mungu; ili kusimamia haki na
amani; ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Waandishi wa habari watambue
dhamana na wajibu wao katika Jamii, daima watafute mafao ya wengi!
habari hii
imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.