Jitambueni kama Familia ya Mungu kwa kudumisha majadiliano, msamaha na upatanisho
ili kujenga haki, imani na matumaini!
Katika Maadhimisho ya Sita ya kuombea amani katika Nchi Takatifu yaliyofanyika Jumapili
iliyopita, tarehe 26 Januari 2014 kwa kuwashirikisha vijana kutoka sehemu mbali mbali
za dunia, waliosali na kuabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa ishirini na manne
na kuhitisha kwa Ibada ya Misa Takatifu, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wametakiwa
kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani.
Katika ujumbe wake kwenye
Maadhimisho haya, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani
anawakumbusha waamini amri mpya upendo, ambayo inawataka kupendana kama Kristo alivyowapenda
wao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea amani kwa Mwaka 2014
umekuwa ni changamoto ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu kama msingi na
njia ya kujenga na kudumisha amani duniani.
Udugu ni msingi wa maisha ya upendo,
amani na mapatano, ikiwa kama utafanyiwa kazi barabara. Utandawazi unaonesha kwamba,
watu wako karibu, lakini kwa bahati mbaya wamemezwa mno na ubinafsi na utamaduni wa
kutojali mahangaiko ya wengine kiasi kwamba; changamoto kwa waamini na watu wenye
mapenzi mema kujenga mshikamano wa kidugu kwa kukpokeana, kukubaliana na kusaidiana
na kwamba, kwa njia ya Kristo wote wanafanyika kuwa ni ndugu wamoja; watoto wa Familia
ya Mwenyezi Mungu, wanaosaidiana.
Vita, kinzani na migogoro bado inaendelea
kutawala sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa anasema Kardinali Turkson haliwezi kukaa
kitako na kuangalia mambo yakienda kombo, bali litaendelea kuonesha mshikamano wa
dhati na waathirika kwa kuwaonjesha upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa
lake; kwa kuendelea kusali ili kumwomba Mfalme wa amani aweze kuwakirimia amani wananchi
wanaoishi kwenye Nchi Takatifu, ili waishi kwa amani na udugu.
Wananchi watambuane
kama ndugu na kusaidiana kwa hali na mali; wakijitahidi daima kufanya kazi kwa pamoja
ili kufikia utimilifu wa maisha ya mwanadamu na utulivu kwa wote. Waamini wajisikie
kwamba, Kanisa ni Familia ya Mungu kwa kujenga na kudumisha majadiliano, msamaha na
upatanisho unaopania kujenga na kuimarisha haki, imani na matumaini. Kardinali Turkson
anawataka vijana kuwa ni mashahidi wa Injili ili amani iweze kuwafikia watu wengi
zaidi.