2014-01-28 07:19:12

Baraza la Makanisa Ulimwenguni lafanya tafakari ya kina kuhusu ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya kuombea amani 2014


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, hivi karibuni aliwaongoza wajumbe wajumbe kutoka dini na makanisa mbali mbali kutafakari kuhusu ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea Amani duniani kwa Mwaka 2014, uliokuwa unaoongozwa na kauli mbiu “Udugu ni msingi na njia ya Amani”. RealAudioMP3

Ni ujumbe unaowachangamotishwa watu wa mataifa kuondokana na chuki, kinzani na uhasama; mambo yanayoendelea kusababisha maafa na majanga mbali mbali katika maisha ya mwanadamu.

Tafakari hii iliandaliwa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva pamoja na Jimbo Katoliki la Lausanne, Geneva na Fribourg. Dr. Tveit anasema, Papa Francisko anawaalika watu wa mataifa kujenga umoja, udugu na mshikamano, kwa kutambua kwamba, wao kimsingi wanaunda familia moja ya binadamu. Watu wakishirikiana katika umoja na udugu, haki na Amani vinaweza kupatikana.

Wajumbe wamempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na kujali mahangaiko ya wananchi wa Syria na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Dhana ya haki na amani, kamwe haiwezi kuelea katika ombwe, bali ni mchakato unaopaswa kufanyiwa kazi kila siku ya maisha ya mwanadamu. Ni changamoto kwa Makanisa kuhakikisha kwamba, yanasimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani katika sehemu mbali mbali za dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.