Wadau wa michezo simameni kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kiroho
na kiutu pamoja na amani Barani Afrika!
Michezo ni chombo cha amani na ina mchango mkubwa katika mchakato wa mapambano dhidi
ya baa la umaskini duniani, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe
wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014.
Maendeleo ya sayansi
na teknolojia ya mawasiliano yanaiwezesha dunia kushikamana na kushirikishana karama
mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wengi. Ikiwa kama Jamii itakiuka dhamana hii kwa
kujikita zaidi katika kutafuta utajiri na faida kubwa, kunahatari kwamba, michezo
ikapoteza fursa ya kuwa ni chombo cha kuelimisha.
Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa
na Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican na kusomwa kwa niaba
yake na Padre Joseph Ballong, wakati wa mkutano mkuu wa saba wa Shirikisho la Vituo
vya Radio Barani Afrika, uliofunguliwa tarehe 27 Januari na unakamilika tarehe 28
Januari 2014, huko Yaounde, Cameroon.
Anasema, inatia moyo kuona kwamba, Vituo
vya Radio Barani Afrika vinaanza kununua leseni ya kuweza kutangaza matukio makubwa
ya michezo kimataifa, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wadau wa michezo
wanasimama kidete kulinda, kutetea na kurithisha tunu msingi za maisha ya kitu na
kiroho, ili kujenga Jamii inayosimikwa katika haki, amani na utulivu, kwani michezo
inatumia lugha ya kimataifa inayovuka mipaka ya kidini, kikabila na kisiasa. Michezo
ina uwezo wa kuwaunganisha watu, kwa kukoleza majadiliano ya kina na ukarimu.
Ni
matumaini ya Padre Lombardi kwamba, michezo itasaidia kuchangia majiundo endelevu
ya haki na amani Barani Afrika na kwamba, Radio Vatican itaendelea kuwa ni mdau mkuu
wa utangazaji wa amani sehemu mbali mbali za dunia.