Utengano kati ya Wakristo bado ni kashfa katika ushuhuda wa Uinjilishaji!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu
Paulo, mwalimu na mtume wa mataifa, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo
tarehe 25 Januari, ameongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Paulo, nje ya kuta za Roma. Ibada hii imehudhuriwa na wawakilishi kutoka madhehebu
mbali mbali ya Kikristo.
Tafakari ya mwaka huu iliandaliwa na Jumuiya ya Wakristo
kutoka nchini Canada, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Je, Kristo amegawanyika?” Hii ndiyo
kashfa ya utengano miongoni mwa Wakristo wanaoungama imani moja kwa Yesu Kristo mkombozi
wa ulimwengu.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amewataka Wakristo
kama ilivyokuwa kwa nyakati za Mtakatifu Paulo kujitahidi kuungana pamoja kwa njia
ya mawazo na maneno na kwamba, umoja huu si mkakati wa kibinadamu bali ni changamoto
kutoka kwa Kristo mwenyewe, anayewavuta wafuasi wake kuungana sanjari na kujiachilia
mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake yanayojikita
katika upendo kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye kiini, sababu na kikolezo cha umoja
miongoni mwa Wakristo.
Utengano miongoni mwa Wakristo si jambo la kawaida anasema
Baba Mtakatifu Francisko, linalohitaji kufanyiwa marekebisho ya kina, kwani utengano
kati ya Wakristo una madhara makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Unahatarisha ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo duniani.
Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo ndiye msingi wa Kanisa na urithi wa wakristo
wote. Lakini inasikitisha kuona kwamba, bado Wakristo wenyewe wamegawanyika kinyume
kabisa cha utashi wa Kristo mwenyewe na utengano huu unaendelea kuwa ni kielelezo
cha kashfa ya ushuhuda wa utangazaji wa Injili duniani.
Baba Mtakatifu anawatia
shime Wakristo kufanya hija pamoja na kutegemezana ili kujenga na kuimarisha umoja
miongoni mwa Wakristo. Hii ndiyo dhamana iliyotekelezwa na Papa Yohane wa XXIII na
Yohane Paulo II, waliotambua umoja wa Wakristo, wakawaongoza Waamini wa Kanisa Katoliki
katika hija ya majadiliano ya kiekumene, kiasi kwamba, miaka hamsini iliyopita, Papa
Paulo VI akaweza kukutana na kukumbatiana na Patriaki Athenagora wa Costantinopoli.
Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya Wakristo, ili kuhakikisha kwamba, wanatembea
pamoja na kujenga mchakato wa majadiliano ya Kiekumene ili kufikia lengo la umoja
kamili kadiri ya mapenzi ya Kristo.
Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene,
dhana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro imejidhihirisha wazi, mwaliko wa kuendelea kufahamiana
zaidi kwa ajili ya majadiliano ya Kiekumene kwa kutambua utume wa Khalifa wa Mtakatifu
Petro, hata kwa siku za usoni.
Changamoto na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza
katika majadiliano ya Kiekumene ni mambo ambayo hayawezi kufichika, lakini kuna haja
kwa Wakristo wapige kupiga moyo konde na kuanza kujivika utashi wa Kristo kwa ajili
ya umoja miongoni mwa Wakristo. Wawe tayari kuvuka vikwazo vyote vinavyosababisha
utengano na hivyo kujivika nguvu ya upendo inayotolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili
ya Kanisa.