2014-01-27 07:55:58

Ushiriki wa Familia ya Mungu katika maandalizi ya maisha ya ndoa na familia!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kwa mara nyingine tena karibu katika kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani. Baada ya kutazama juu ya maandalizi ya kuingia katika maisha ya ndoa na juu ya waoanaji wenyewe kuyapa hadhi maisha yao kwa kujiwekea miiko mbalimbali ya maisha. RealAudioMP3

Katika kipindi hiki tuangazie kwa ufupi juu ya ushiriki wa jamii nzima katika kuwasaidia wanandoa wapya hawa kuanza maisha ya ndoa kwa mwondoko wenye matumaini, utakaowafikisha mbali katika safari yao ya agano; ambayo ni safari ya kijamii na safari ya kiroho pia; yenye lengo la kuwafikisha mbinguni.

Miiko ni nidhamu ya maisha. Kuna wakati inauma, lakini husaidia sana kuzuia hatari mbalimbali ambazo zingeweza kuiyumbisha familia. Na leo, tujitazame sote kama jamii ya watu ambamo hawa wanandoa wametoka. Tuwasaidieje ili waanze vizuri, wakue, na wasitawi katika agano lao. Jamii tunaweza kuwasaidia katika mengi kama vile:-
Mosi; TUWAOMBEE! Msaada wa kwanza kabisa au zawadi ya kwanza ambayo tunaweza kuwapa wanandoa ni SALA. Tuwaweke mikononi mwa Mungu kwa njia ya sala, ili yule mwovu asiwapepete na kuwamaliza. Hata pale tunapoona “WAMETINDIKIWA DIVAI”, divai ya upendo, divai ya amani, divai ya maelewano mema, divai ya kuvumiliana, divai ya uaminifu, divai ya uwajibikaji nk, Ni sisi jamii ya waamini na wanandugu, ndio tunaopaswa kuchukua nafasi ya Mama wa Yesu katika Arusi ya Kana [Yoh. 2:1-11]; kuwaombea hawa maharusi wetu kwa Bwana tukisema “hawana divai”. Ni kwa msaada wa sala zetu, tunaweza kuwasaidia hawa ndugu wakaendelea mbele zaidi katika safari yao ya agano.

Zawadi ya sala, huanza tangu mwanzoni kabisa siku wanapofunga ndoa. Na hapa, kichungaji tuhimize jambo mmoja; ni vema zaidi watu tukajifunza na tukapenda kuhudhuria ile ibada au misa ambamo hawa maarusi wanaweka agano lao la ndoa. Tunapokutanika pamoja mahali pa Ibada, kuinua sala zetu kwa pamoja kwa Mungu ili kuwaombea huruma na msaada wake, hakika Mungu atasikia kilio chetu. TUNASEMA TENA HILI LITAZAMWE KICHUNGAJI.

Ni aibu sana nyakati zetu; sehemu inayohusu Ibada kwa Mungu ambapo hawa ndugu zetu wanamwahidia Mungu kwa kiapo; watu wachache sana wanahudhuria. Ila kwenye ibada za tumbo, yaani kwenye sherehe, kumbi zinakuwa zimejaa mno. Na hakuna sababu ya msingi ya kutohudhuria Ibada; NI KUPUUZIA TU, KUTOONA UMUHIMU. Ni wakatoliki walewale, pengine na wana ndugu pia, hawana msukumo wa kwenda kushiriki IBADA YA NDOA KANISANI; Ila wana muda mwingi sana wa kushiriki kula tu basi! Eti wanakula michango yao! Hili tulitazame na kulirekebisha kabla halijawa utamaduni wetu.

Pili, TUWASHAURI: Ushauri ni paji kutoka kwa Bwana. Sio kila mwenye mdomo anafaa kutoa ushauri. Sio kila mwenye umri mkubwa au elimu kubwa ana hekima na busara ya kutoa ushauri. Hekima pia ni paji kutoka kwa Bwana. Endapo UTAOMBWA KUTOA USHAURI, nawe mwenyewe unaona unastahili kufanya hivyo ili kuboresha maisha ya wanandoa, basi fanya hivyo kwa busara kubwa huku ukiwa na MACHO MAKUBWA NA KIFUA KIPANA. Yaani, kwa macho makubwa, uwe na ule uwezo wa KUTAZAMA SHIDA HALISI YA WANANDOA HAWA kwa mapana yake, pasipo kuwa na hila wala upendeleo. Tazama tatizo ili uwe msaada. Ukiwa na macho madogo, yaani ukiwa mfinyu katika kupembua mambo, utatazama tatizo na kulitatiza zaidi. Tena uwe na KIFUA KIPANA, yaani UWE NA UWEZO WA KIUTU UZIMA WA KUTUNZA SIRI. Sio watu wamekushirikisha mambo yao ya ndani kabisa ya ndoa; wewe unapita kuyaimbaimba mtaani na kumsimulia kila mtu; HAIPENDEZI.

Mpenzi msikilizaji wa Radio Vatican, kwa leo tunatua nanga, ili nipate nafasi ya kukuandalia tena ”mabango” kwa makala ijayo, tutakapoendelea kuhekimishana umuhimu wa kuwapatia wanandoa nafasi, namna ya kutawala na kudhibiti midomo yetu na zaidi ya hayo kutakiana mema, kwani kuna baadhi ya watu wana roho ya kwanini!

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi
Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.