Mshikamano wa Papa Francisko na wagonjwa wa Ukoma duniani!
Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro,
Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha waamini kwamba, Jumapili ya tarehe 26 Januari,
Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa inaadhimisha Siku ya Wagonjwa wa Ukoma Duniani.
Huu
ni ugonjwa unaoonekana kuanza kutoweka, lakini bado unaendelea kusababisha madhara
makubwa kwa watu. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu ni kuendelea kuonesha mshikamano
na wagonjwa wa Ukoma sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawahakikishia sala
na uwepo wake wa karibu na anaendelea kuwaombea wote wanaojihusisha na huduma kwa
wagonjwa wa Ukoma.
Baba Mtakatifu ameelekeza sala zake nchini Ukraine ambako
kwa sasa hali ni tete kutoka na machafuko ya kisiasa na kijamii ambayo yamepelekea
hadi sasa watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya wakati wa mapambano
kati ya Jeshi la Polisi na wanaharakati nchini humo wanaodai Ukraine ijiunge na Umoja
wa Ulaya. Baba Mtakatifu anawataka wahusika kujenga utamaduni wa majadiliano kati
ya Serikali na raia pamoja na kukomesha vitendo vya uvunjifu wa amani, ili kujenga
moyo wa amani kwa ajili ya mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka
kwa namna ya pekee Cocò Campolongo, mtoto wa miaka mitatu aliyeuwawa kikatili miaka
mitatu iliyopita kwa kuchomwa moto ndani ya gari huko Cassano, kitendo cha kusikitisha
sana na mwaliko kwa wahusika kutubu na kuongoka.
Baba Mtakatifu amewakumbuka
pia wananchi kutoka Mashariki ya mbali, yaani China, Korea na Vietnam wanaojiandaa
kuadhimisha Mwaka Mpya. Anawatakia furaha na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu
katika maisha ya kifamilia. Wajitahidi kujenga na kudumisha dunia inayosimikwa katika
utu, ili amani iweze kutawala.
Baba Mtakatifu amemtaja Mtumishi wa Mungu Maria
Cristina aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri Jimbo kuu la Napoli. Ni Malkia wa Visiwa vya
Sicilia; aliyeishi kwenye Karne ya kumi na tisa. Mwanamke aliyekuwa na utajiri mkubwa
wa maisha ya kiroho, mnyenyekevu na aliyeguswa na mahangaiko ya jirani zake, kiasi
kwamba, akatambulikana na wengi kuwa ni Mama wa Maskini. Hiki ni kielelezo makini
cha upendo kinachoonesha kwamba, maisha ya Kiinjili yanawezekana kutolewa ushuhuda
katika medani mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru
kwa namna ya pekee Chama cha Vijana Wakatoliki waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na wazazi na walezi wao.