2014-01-27 09:42:04

Hija ya kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Austria


Baraza la Maaskofu Katoliki Austria, kuanzia tarehe 27 hadi 31 Januari 2014 linafanya hija ya kitume, mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi mbali mbali wa Mabaraza ya Kipapa. Kanisa Katoliki nchini Austria, katika miaka ya hivi karibuni limepitia katika kipindi kigumu na chenye changamoto nyingi za shughuli za kichungaji.

Idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki imepungua na kufikia asilimia 63.4% ikilinganishwa na asilimia 89% kunako mwaka 1962. Waamini wengi walishikwa na ubaridi wa imani kiasi kwamba idadi ya wale waliokuwa wanahudhuria kwenye Ibada ya Misa Takatifu walipugungua, kiasi kwamba, Makanisa yalibaki matupu!

Yote haya yalisababishwa na utengano kati ya Wakatoliki, kashfa za nyanyazo za kijinsia dhidi ya watoto wadogo; baadhi ya Wakristo walijitokeza hadharani kuwashutumu viongozi wa Kanisa kwa kulipeleka Kanisa mrama kinyume cha utashi wa Kristo mwenyewe.

Hili ni kundi la Waamini waliotaka Kanisa Katoliki nchini Austria kufuata mchakato wa mageuzi ulioanzishwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kujikita katika: majadiliano, nafasi ya wanawake ndani ya Kanisa; kuhusu Ekaristi kwa Jumuiya nzima ya Waamini pamoja na ushiriki wa wanandoa walioachana na kuoa au kuoana tena.

Waamini hao walitaka useja ndani ya Kanisa liwe ni jambo la hiyari; mapadre walioacha na kuoa waruhusiwe kulihudumia tena Kanisa; watu wenye mwelekeo wa ushoga walibaguliwe wala kutengwa. Waamini walilitaka Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Madai haya yalikuwa ni mazito na tete kwani yaligusa kwa undani zaidi Mafundisho, maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Maaskofu Austria kunako Mwaka 1998 likaitisha mkutano wa kitaifa ili kujadili mustakabali wa Kanisa Katoliki nchini Austria kwa kujikita katika upatanisho na kuendeleza majadiliano kati ya viongozi wa Kanisa na Waamini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Familia ya Mungu katika ujumla wake. Maaskofu wakatoa angalisho kuhusu mambo yaliyokuwa yanasigana kimsingi na Mafundisho ya Kanisa Katoliki kwa kufafanua msimamo wa Kanisa.

Kanisa Katoliki nchini Austria liliendelea kujielekeza katika majadiliano katika: uwazi na ukweli katika mkutano wake uliofanyika kunako mwaka 2013, kama sehemu ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia na Uinjilishaji, inayotarajiwa kuadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba 2014. Waamini na watu wenye mapenzi mema wamechangia mawazo yao ili kufanikisha mikakati inayoweza kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Watu wameguswa kwa namna ya pekee na mchakato wa majadiliano ulioanzishwa na Kanisa kwa kuwashirikisha waamini hata katika masuala nyeti ya maisha na utume wa Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.