Uwajibikaji kimaadili ni jambo muhimu katika kupambana na athari za mabadiliko ya
tabianchi!
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuweka mikakati makini katika masuala ya fedha na
uchumi ili kukabiliana kwa dhati kabisa na changamoto ya athari za mabadiliko ya tabianchi
yanayoendelea kusababisha majanga makubwa katika sehemu mbali mbali za dunia. Hili
ndilo jukumu linalopaswa kushughulikiwa na wajumbe wa Jukwaa la Uchumi Duniani huko
Davos, nchini Uswiss, unaofungwa rasmi tarehe 25 Januari 2014.
Jukwaa la Uchumi
Duniani, lilikuwa linaongozwa na kauli mbiu "Kuleta mabadiliko duniani: athari zake
kwa Jamii, Kisiasa na Kibiashara". Dr. Olav Fykse Tveit, katibu mkuu wa Baraza la
Makanisa Ulimwenguni anasema, Makanisa yanaunga mkono mchakato unaopania kujenga haki
katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, kuna haja kwa wanasiasa na wachumi
kushirikiana kwa pamoja ili kukabiliana na athari zinazoendelea kujitokeza kabla ya
mambo hayajaharibika zaidi.
Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zilikwamisha
mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na maafa yanayosababishwa na athari
za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali duniani. Mkakati huu hauna budi kuwashirikisha
wadau mbali mbali kwa kuanzia kwa: Serikali, taasisi za fedha na biashara; vyama vya
kiraia na Mashirika ya Kidini.
Jumuiya ya Kimataifa anasemam Dr. Tveit haina
budi kurejesha tena imani na matumaini katika taasisi za kidemokrasia, ambazo nyingi
kwa sasa zinaanza kupoteza dira na mwelekeo wake, kwa kutekeleza ahadi zake katika
Jumuiya ya Kimataifa. Mchango wa Makanisa na Taasisi za Makanisa ni jambo la msingi,
linalohitaji kuzingatia kanuni maadili na uwajibikaji katika maamuzi kuhusu taasisi
za fedha na biashara.
Wadau mbali mbali wanaendelea kuyapongeza Makanisa kwa
kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kusababisha majanga makubwa sehemu mbali
mbali za dunia. Lengo ni kuiwezesha Jamii kudumisha haki katika masuala ya mabadiliko
ya tabianchi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon amewahimiza
viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Taasisi za Fedha na Biashara kushikamana
katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.