2014-01-25 07:49:00

Nendeni mkajifunze kusikiliza kilio cha damu!


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea mahojiano maalum kuhusu Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspar, Itigi, Singida. Katika studio za Radio Vatican tunaye Padre Serafin Lesiriam, Mkurugenzi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar. Anafafanua kuhusu wazo la kujenga Chuo, mikakati ya kukipanua, changamoto na mipango endelevu iliyoko kwa sasa. RealAudioMP3

Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S lililoanzishwa na Mtakatifu Gaspar del Bufalo tarehe 15 Agosti, 1815, ni Shirika la Kazi za Kitume linaloongozwa na kifungo cha upendo, maisha ya kijumuiya, tasaufi ya damu Azizi ya Yesu na huduma ya Neno la Mungu, ambayo kimsingi ni Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Shirika hili tangu lilipofika nchini Tanzania, mara baada ya vugu vugu la maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili, limekuwa likijitahidi wakati wote huo, kusoma alama za nyakati, kwa kusikiliza kwa makini kilio cha damu hasa miongoni mwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wamejitahidi kuifuta ile Njia ya Msalaba, ili kuwamegea watu tumaini jipya linalofumbatwa katika hekima ya Msalaba.

Daima Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, wamekuwa mstari mbele katika kushiriki kwenye mchakato unaopania kumletea mwanadamu maendeleo endelevu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Huduma ya maji safi na salama sehemu mbali mbali, hasa zile kame nchini Tanzania ni kati ya mafanikio makubwa yaliyofanywa na Wamissionari hawa katika sekta ya maji; hawako nyuma katika utoaji wa elimu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kuzitegemeza familia zao kwa njia ya elimu makini hususan katika ufundi. Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wamejitoa bila ya kujibakiza hasa zaidi katika sekta ya afya, kielelezo hai ni Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Singida, Tanzania.

Leo ninapenda kuelezea kwa uchache historia fupi ya Chuo, changamoto na mipango endelevu tuliyo nayo kwa sasa na kwa ajili ya siku za usono. Chuo cha uuguzi cha Mt. Gaspar ni Chuo kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki na kuongozwa na kumilikiwa na Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu, C.PP.S.

WAZO LA KUJENGA CHUO


Kwa kuangalia na kutambua mahitaji ya wakati wa sasa kirho na kimwili Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu liliamua kujenga chuo hiki.Uamuzi huu mzuri ulisukumwa kwa kiasi kikubwa na mambo makuu mawili:

    Upungufu mkubwa wa watumishi wa afya hasa katika kada ya uuguzi. Si upungufu wa kiidadi tu bali hata wa watumishi wenye taaluma, maadili, uwezo na wanaojiamini katika fani yao ya uuguzi katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kupambana na changamoto mbali mbali hususan katika sekta ya afya na tiba ya mwanadamu.


    Malengo ya kitaifa ya maendeleo ya Milenia yanayo lidai taifa la Tanzania kutoa huduma ya afya ya maendeleo ya msingi ( The Primary Health Services Development 2007-2010). Maazimio hayo yalipelekea Tanzania kujenga katika kila kijiji Zahanati na kila kata kuwa na Kituo cha afya. Matokeo yake ni kuwa na upungufu mkubwa wa wauguzi wa kutoa huduma katika zahanati hizo na vituo hivyo vya afya. Shirika liliamua kuchangia katika kujibu kilio hiki kikubwa cha watumishi katika sekta ya afya, jambo hili si lelemama kwani lina gharama na mahitaji yake.



Hivyo tarehe 04.09.2006 chuo kilifunguliwa rasmi. Chuo hiki kinaendeshwa kwa kufuata taratibu, kanuni. maadili na sera za Kanisa Katoliki (Baraza la Maaskofu Katoliki TEC), Wizara ya Afya na Baraza la Mitihani la Taifa.

Wazo msingi si kupata wauguzi tu bali kuwapata wauguzi bora na wenye maadili ya kufanya kazi aliyoifanya Yesu Kristo mwenyewe ya kumponya mwanadamu kiroho na kimwili: kiroho kwa kumwondolea dhambi zake na kimwili kwa kumponya magonjwa na kero nyingine za maisha.

Ndiyo maana Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, hivi karibuni katika ujumbe wake kwa Siku ya wagonjwa duniani, anakazia umuhimu wa Sakramenti za uponyaji kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Hii inajionyesha katika kauli mbiu ya chuo TUFANYE MENGI,VIZURI NA HARAKA. Haya ni maneno ya Mtakatifu Gaspar, ambaye yamekuwa ni kati ya kauli mbiu na dira katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Jamii.

KUANZA KWA CHUO NA KUPANUKA KWAKE


Chuo kilipoanza hapo tarehe 04.09.2006 hakikuwa na majengo yake wala hakikuwa na miundo mbinu yote katika ukamilifu wake. Hivyo kwa sehemu kubwa ya chuo kilitumia majengo ya hospitali ya Mt. Gaspar. Tarehe 16.03.2007 liliwekwa jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya chuo na Mheshimiwa Pd. Giovanni Francillia aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wa wakati ule na jiwe hili lilibarikiwa na Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Singida, Tanzania kwa wakati huo. Kwa sasa chuo kina majengo yake yenyewe yaliyofunguliwa rasmi mwezi Septemba 2010.

Chuo kilipoanza kilikuwa na walimu 3 na watumishi wengine (supporting staffs) 8. Kwa sasa chuo kina walimu 7 wa kudumu na 10 wa muda na watumishi wengineo 13.

Chuo kilianza na wanachuo 40 mwaka 2006 wakati mwka 2011 tumefikisha idadi ya wanachuo 200. Upanukaji wa chuo hiki unatokana na kupanuka kwa mahitaji na ubora wa chuo katika kutoa mafunzo yake.Chuo kilipoanza kilikuwa kinatoa kozi ya Uuguzi kwa kuwapandisha wauguzi waliopo makazini lakini wakiwa na mafunzo ya ngazi ya cheti hivyo kuwapatia mafunzo ya kuwapandisha kuwa wauguzi wa ngazi ya stashahada. Jambo hili halikuwa suluhisho la kupunguza uhaba wa watumishi wauguzi bali lilikuwa suluhisho la kuwaongezea ujuzi wauguzi na hivyo kufanya kazi kwa ujuzi na kujiamini zaidi.

Mwezi Mei mwaka 2009 Mheshimiwa Jakaya Mrisho kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipotembelea Itigi alifika katika Hospitali ya Mt. Gaspar na kufungua nyumba za kuishi madaktari, katika hotuba yake alituomba tuongeze idadi ya wanachuo. Uongozi ulilipokea ombi hili kama changamoto na kuanza kulifanyia kazi.

Hivyo, mwezi Septemba mwaka 2010 tuliongeza idadi ya wanachuo kuingia kwa mwaka kutoka 50 na kuwa 100. Tulianza kuchukua wanachuo ambao hawana taaluma ya uuguzi na kuwapatia kozi ya miaka mitatu na hvyo kuhitimu mafunzo ya uuguzi kwa ngazi ya Stashahada. Hivyo kwa sasa chuo kinao wanachuo wa kozi ya Uuguzi kwa ngazi ya Stashahada kwa kozi ya mwaka mmoja na kwa kozi ya mika mitatu.

Tunapenda kuwashukuru wale wote waliochangia na wanaoendelea kuchangia kuendeleza chuo hadi kufikia hapo kilipo. Tangu mwaka 2006 wamahitimu wanachuo 200 na wote wamefaulu vizuri sana. Lakini, haitoshi kufaulu vizuri kiasi hiki, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanazingatia maadili ya kazi, utu, heshima na maisha ya mwanadamu yakipewa kipaumbele cha kwanza kabisa. Wao wanapaswa kuwa ni mabalozi wema na waaminifu wa Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspar, Itigi.

CHANGAMOTO


Changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo chetu ni kama ifuatavyo:
    Upungufu wa walimu kulingana na idadi ya wanachuo tulionao hivi sasa. Tunapaswa kufikia malengo ya kuwa na mwalimu mmoja kwa kila wanachuo 10.
    Ukosefu wa wanachuo wenye sifa za kujiunga na chuo. Bado kuna tatizo kubwa la kuwapata wanachuo wenye sifa kujiunga na chuo. Mtu anayependa kujiunga na chuo lazima awe amefaulu masomo matatu ya sayansi. Hili bado ni tatizo la kitaifa.
    Uhaba wa vifaa kwa ajili ya mafunzo ya vitendo. Tunalo bado tatizo kubwa la kupata vifaa toshelezi ili kuweza kukifanya chuo kifikie ngazi inayokubalika hata kimataifa kwa utoaji wa mafunzo ya uuguzi.
    Gharama za uundeshaji kupanda mwaka hadi mwaka tena kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na gharama za ada.
    Wanachuo kushindwa kulipa ada kutokana na hali duni ya kipato cha familia wanakotoka.


MIPANGO ENDELEVU


    Kukipanua chuo kwa kutoa mafunzo hadi kufikia ngazi ya shahada. Aidha hata kuweza kutoa kozi nyingine zinazo hitajika kama maabara.
    Kukiunganisha chuo na vyuo vingine vya ndani na hata nje ya nchi kuweza kuwa na mbadilishano wa mafunzo.
    Kukiwekea mtandao wa mawasiliano wa uhakika utakaowezeha kuwarahisishia wanachuo kujisomea kwa njia ya interne.
    Kuongeza majengo ya chuo ili kuendena na mahitaji halisi na ukuaji wa Chuo chenyewe.









All the contents on this site are copyrighted ©.