2014-01-25 15:19:58

Mshikamano wa upendo na wananchi wa Ufilippini kutoka kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko amemtuma Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, kumwakilisha nchini Ufilippini, ili kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwake kwa ajili ya wananchi wa Ufilippini waliokumbwa na tufani iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao hivi karibuni.

Ziara hii ya mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu inaanza rasmi tarehe 26 Januari hadi tarehe 31 Januari 2014. Akiwa nchini humo, Kardinali Robert Sarah atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini. Anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Benigno Aquino III na baadaye, atatembelea maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi kwa tufani.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Cor Unum anachangia ujenzi wa Kituo kipya cha kulelea watoto yatima pamoja na nyumba moja ya wazee. Katika eneo hili, kutajengwa pia nyumba ya watawa, Kikanisa na Zahanati kwa ajili ya matibabu ya watu watakaokuwa wanahudumiwa hapo. Hiki ni kielelezo cha imani katika matendo.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Ufilippini hivi karibuni zinazonesha kwamba, watu zaidi ya 5, 500 walifariki dunia; wengine 26, 000 walijeruhiwa na zaidi ya watu 2, 000 hawajulikani mahali walipo! Inakadiriwa kwamba, watu millioni 3. 8 hawana makazi. Kimsingi zaidi ya watu millioni 12 wameathirika kutokana na tufani hiyo.

Wasi wasi mkubwa kwa sasa ni kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko. Cor Unum imechangia kiasi cha dolla za kimarekani 150, 000 kwa ajili ya kutoa msaada wa dharura kwa watu walioathirika. Mashirika mbali mbali ya misaada ya Kanisa Katoliki yanaendelea kutoa huduma kwa waathirika nchini Ufilippini.







All the contents on this site are copyrighted ©.