Majadiliano kati ya Kanisa na Serikali ya Ufaransa ni muhimu kwa ajili ya mafao ya
wengi!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 24 Januari 2014 amekutana na kuzungumza na
Rais Francois Hollande wa Ufaransa na baadaye alikutana na kuzungumza na Kardinali
mteule Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu
Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na uhusiano wa kimataifa mjini
Vatican.
Katika mazungumzo, viongozi hawa wawili wamegusia mchango wa Kanisa
katika kutafuta mafao ya wengi nchini Ufaransa; uhusiano kati ya Ufaransa na Vatican
pamoja na umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kina kati ya Kanisa na Serikali, ili
kujenga na kudumisha ushirikiano katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ufaransa
katika ujumla wao.
Viongozi hao wamejadili pia umuhimu wa kusimama kidete
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu katika masuala ya: ndoa na familia;
maadili katika tafiti; umuhimu wa kuheshimu na kuthamini uhuru wa kidini pamoja na
kutoa ulinzi kwa maeneo na nyumba za Ibada.
Baba Mtakatifu Francisko na mgeni
wake Rais Hollande katika masuala ya kimataifa wamezungumzia; baa la umaskini, maendeleo
na utunzaji bora wa mazingira. Vita na kinzani huko Mashariki ya kati na katika baadhi
ya nchi Barani Afrika ni mambo ambayo yamezungumziwa kwa kina na mapana. Viongozi
hawa wamekazia umuhimu wa kudumisha msingi wa majadiliano ya kweli kama njia ya kujenga
umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na watu kuheshimiana na kuthaminiana hata katika
tofauti zao za kidini na kikabila.