Cheche za mafanikio ya majadiliano ya kiekumene zaanza kuonekana!
Je, Kristo amegawanyika? Ndiyo kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Juma la Kuombea
Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2014. Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la
kuhamasisha Umoja wa Wakristo anabainisha kwamba, majadiliano ya kiekumene yameendelea
kupewa kipaumbele cha pekee na Kanisa Katoliki tangu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican.
Kanisa ambalo kimsingi ni: moja, takatifu, katoliki
na la mitume, kwa asili linajikita katika umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, lakini
kwa bahati mbaya, bado kuna utengano miongoni mwa wafuasi wa Kristo, jambo ambalo
ni kashfa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliiona na kusikitishwa na kashfa
hii inayoendelea kujionesha miongoni mwa Wakristo.
Ndiyo maana, Miaka 50 iliyopita,
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakachapisha hati kuhusu majadiliano ya
Kiekumene inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Unitatis Redintegratio”, ambayo
mwaka huu inaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipochapishwa. Wakristo wanatamani
kuona Kanisa la Mungu moja na linaloonekana, liwe kweli ni kwa ajili ya wote na linalotumwa
duniani kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili watu waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi
Mungu na hatimaye, kupata ukombozi ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mgawanyiko
miongoni mwa wafuasi wa Kristo ni jambo ambalo linakwenda kinyume cha mapenzi ya Kristo
mwenyewe aliyewaombea wafuasi wake wawe wamoja kama Yeye na Baba yake wa mbinguni
walivyo wamoja! Kardinali Koch anasema, utengano miongoni mwa Wakristo unachafua utakatifu
wa maisha ya Kanisa na kuvuruga ushuhuda wa utangazaji wa Injili ya Kristo kwa watu
wa Mataifa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliona na kutambua kwamba,
majadiliano ya kiekumene ni kati ya vipaumbele vya Kanisa Katoliki katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Kanisa Katoliki linatambua na kuthamini dhamana
na utume wa majadiliano ya kiekuemene mintarafu uelewa wa Kanisa kama Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Vatican wanavyofafanua kwa kina katika hati juu ya Kanisa, Lumen Gentium,
yaani Mwanga wa Mataifa.
Kuna uhusiano wa dhati kati ya Kanisa na Majadiliano
ya Kiekuemene, kwani hii ni hija ambayo Kanisa Katoliki linapania kusaidia mchakato
wa kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo katika uhalisia wa maisha na
wala si katika dhana wala wazo la kufikirika. Hati juu ya Kanisa inafafanua kwa kina
na mapana mwelekeo huu wa maisha.
Kardinali Kurt Koch anabainisha kwamba, Papa
Paulo VI katika hotuba yake ya ufunguzi wa Awamu ya Pili ya Maadhimisho ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa majadiliano ya kiekumene
katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi kuhusu ufahamu
wa Kanisa ili kuanzisha mchakato wa kuponya madonda ya utengano miongoni mwa Wakristo.
Hati ya Majadiliano ya Kiekumene ilipewa uzito wa pekee sanjari na kuongeza jitihada
za majadiliano ya Kiekumene na Makanisa ya Mashariki pia.
Papa Paulo VI anasema
kwamba, majadiliano ya Kiekumene ni hija ya Mama Kanisa, kama anavyokazia Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili katika hati yake ya kichungaji, ili wote wawe wamoja, Ut Unum
Sint. Huu ni mchakato wa maisha na utume wake, kwa kuendelea kuwa makini ili kusikiliza
sauti ya Roho Mtakatifu kwa Makanisa pamoja na kusoma alama za nyakati.
Baba
Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaivalia njuga changamoto ya majadiliano ya Kiekumene
katika mikakati na vipaumbele vyake kwa maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro. Hii inatokana na ukweli kwamba, majadiliano ya Kiekumene yanapata chimbuko
lake kutoka katika asili ya utume wa Kanisa lenyewe. Ni mchakato unaofumbatwa katika
uhalisia wa maisha katika imani.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake
wa kitume, Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium anasema kwamba, majadiliano ya Kiekumene
si sehemu ya mchakato wa shughuli za kidiplomasia au jambo la kulazimishana, bali
ni changamoto ya kufanya toba na wongofu wa ndani, ili Wakristo kwa pamoja waweze
kushikamana katika kutangaza Injili ya Furaha, ili ushuhuda wao uweze kuwa na mvuto
pamoja na mashiko.
Huu ndio mwendelezo wa Mafundisho wa Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican katika mchakato wa majadiliano ya Kiekumene. Hati za Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Kanisa, Majadiliano ya Kiekumene na Makanisa ya Mashariki
ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, katika mchakato wa ujenzi wa Umoja
wa Kanisa la Kristo.
Kardinali Kurt Koch anaendelea kufafanua kwamba, Sheria
za Makanisa ya Mashariki, zilizoidhinishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kunako Mwaka
1990 ni matunda ya mchakato wa majadiliano ya Kiekumene na Makanisa ya Mashariki ili
kuweza kupata umoja kamili miongoni mwa Wafuasi wa Kristo. Ni mwaliko na changamoto
ya kufanya hija ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kweli.
Ni matumaini
ya Kanisa Katoliki kwamba, mwaka huu 2014 katika Jubilee ya Miaka 50 tangu hati ya
Majadiliano ya Kiekumene ichapishwe na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican,
hatua kubwa zaidi zinaweza kutekelezwa na Makanisa, ili kuponya kashfa ya utengano
kati ya Wakristo. Mwaka 2017, Makanisa ya Kiluteri yatakuwa yanaadhimisha Jubilee
ya Miaka 500 tangu yalipofanya mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa.
Huu ni
mwaliko wa kutoka katika hali ya kudhaniana vibaya na kuanza mchakato wa ujenzi wa
Umoja wa Kanisa, kwa kujikita zaidi katika mambo yanayowaunganisha Wakristo katika
maisha na imani pamoja na kujitahidi kuponya majeraha ya utengano yaliyojitokeza miaka
500 iliyopita.
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza
na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthiodox la Costantinopoli, kama
kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na kuzungumza na
Patriaki Athenegoras Januari 1964. Huu ni mchakato wa majadiliano ya Kiekumene yanayojikita
katika Upatanisho, ili kuungama Imani moja kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanakumbuka
kwa namna ya pekee Mwaka 1054, uliopelekea utengano ulioleta ubaridi katika upendo,
umoja na mshikamano kati ya Wakristo.
Kardinali Kurt Koch anatumaini kwamba,
majadiliano ya Kiekumene yanayoendelea kutekelezwa kati ya Patriaki Bartolomeo wa
kwanza na Baba Mtakatifu Francisko yataweza kuwasha moto mpya wa umoja na mshikamano
wa dhati miongoni mwa Wakristo hasa kwa Wakristo kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi
Takatifu, uwepo endelevu wa Kristo ndani ya Kanisa lake. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
unaendelea kuwa ni nguzo msingi katika mchakato wa majadiliano ya Kiekumene miongoni
mwa Wakristo.