Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Tupo pamoja tena nawe katika jiji la upendo wa Mungu, yaani Neno lake ambalo daima
latupatia uzima na pia latufanya tuwe huru katika maisha yetu kama kweli tunaliishi
na kulifuata kwa unyenyekevu. Ni Dominika ya III ya kipindi cha kawaida cha mwaka
A, kipindi cha matumaini kama ambavyo chajionesha katika mavazi ya Misa Takatifu,
yaani rangi ya kijani.
Masomo tunayoyatafakari
tunayapata katika kitabu cha Isaya 9:1-4, 1Kor. 1:10-13,17 na Injili Mt. 4:12-23.
Masomo haya yanatupa mwaliko wa kuona na kuupokea mwanga wa Kristu unaoanza kuangaza
kuanzia Galilaya, ndiyo kusema Kristo ni nuru na taa ya kuongoza maisha yetu. Nabii
Isaya anatuambia wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu, na wale waliokaa katika
uvuli wa mauti nuru imewaangaza. Tena Isaya anaona watu wanavyofurahi, na hivi anatangaza
kuvunjiliwa mbali nira ya mizigo ya watu na sasa watu hao wameingia katika uhuru kamili
wa wana wa Mungu.
Mpendwa msikilizaji nabii Isaya kama tutambuavyo anaishi
katika karne ya 8 kabla ya Kristo. Nabii Isaya anaagua kwa makabila ya Zabuloni na
Naftali ambayo yako kasikazini mwa Palestina ambayo hivi leo ni Galilaya. Anapotangaza
unabii huu makabila haya yako katika taabu kubwa yaani manyanyaso chini ya Waasiria,
ndiyo kusema wako katika giza. Ni katika mantiki hiyo nabii anaona mwanga katika
ndoto utakaowafikia watu hawa na kuwaweka huru. Mwanga huu utatokea kwanza pale mlimani
Galilaya na polepole utaenea na kuangaza nchi nzima.
Mpendwa msikilizaji,
Isaya ataka kusema nini? Anataka kusema kuwa madhulumu yanayowapata ndugu hawa yatamalizwa
na mwanga huu ambao utaondoa giza lote, na hivi utawala wa Waasiria utakoma. Kwa hakika
mwanga huu ni Kristo Masiha atakayezaliwa na kuanza kuhubiri kuanzia Mlima wa Galilaya.
Itachukua miaka 700 hivi, kumbe lazima kutambua kabisa kuwa namna ya utendaji wa Mungu
ni tofauti na utendaji wetu. Mungu hutunza ahadi yake hata baada ya miaka mingi kupita.
Tukumbuke ahadi aliyompa Ibrahimu. Hivi leo bado kuna machafuko, vita na mambo
kama hayo, je mwanga umekoma kuangaza? Mwanga unaangaza lakini yafaa kufungua macho
katika uhuru wangu na kuuelekea mwanga huo vinginevyo hautanifikia na hivi nitaendeleza
vita na madhulumu katika ulimwengu huu!
Mpendwa msikilizaji, Mtume Paulo anawakemea
Wakorinto ambao wamejenga kuta za migawanyiko na utengano katika jumuiya yao. Ndiyo
kusema wengine wanajiona ni wa Paulo na wengine ni wa Apolo na wengine ni wa Kefa
na mwishoni wengine ni wa Kristo! Tena mbaya zaidi katika kumega mkate na kunywea
kikombe cha divai kila mmoja anafanya peke yake katika kona! Si hayo bali wamejawa
na fitina, wivu na kuhukumiana kusikoisha na pia kusikokuwa na miguu wala mikono.
Basi katika haya Mtume Paulo anaanza mafundisho yake akisema Kristo hajagawanyika,
ni yuleyule wa jana na leo na daima katika umungu wake. Kwa jinsi hiyo anawaonya na
kuwafundisha wakaishi na kupalilia umoja katika jumuiya yao, kwa maana wahubiri wote
wa Neno la Mungu yaani Mtakatifu Petro, Apolo na yeye mwenyewe na watakaofuata wanahubiri
Neno lilelile ambaye ni Kristu mwenyewe, chimbuko la umoja katika jumuiya.
Anazidi
kuwaambia kuwa wahubiri wote ni watumishi katika shamba la Bwana na wala si mabwana
katika Kanisa. Mpendwa mwana wa Mungu jambo la utengano liliwapata Wakorinto, je sisi
tuko nje ya shida kama hiyo? Kwa hakika jumuiya zetu, familia na mahali pa kazi kuna
misukosuko na malumbano na wivu, kumbe yafaa yote kuyasuruhisha tukimtazama Kristu
mwanga na chanzo cha maisha yetu.
Katika Injili tunapata kumwona Yesu Kristu
katika shughuli za kichungaji huko Kapernaumu, mji ulio pwani, mipakani mwa Zabuloni
na Naftali yaani katika Galilaya. Kuwa kwake pale ni ili litimie lile neno alilolinena
nabii Isaya: Watu wa Zabuloni na Naftali, waliokaa katika giza wameuona mwanga mkuu,
mwanga mkuu umewazukia.
Jambo gani anafanya huko ni lile la kutangaza uhuru
na ukombozi toka katika uvuli wa mauti. Kauri mbiu ya mahubiri yake huko ni “Tubuni
kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia” Mpendwa msikilizaji wakati huohuo akihubiri
atawaita na kuwachagua watu kadhaa kwa ajili ya kuingia katika seminari yake wakiandaliwa
kwa ajili ya utume wa kuhubiri habari njema.
Tunatambua kuwa Bwana mwenyewe
ndiye chanzo cha kila jema ukiwamo wito kwa awaye yote. Wito ni zawadi toka kwa Mungu.
Kristu yuko huko kadiri ya injili ya Matayo akianza utume wake hadharani pale katika
milima ya Galilaya. Mwanga ule tuliousikia katika somo la kwanza ndo huu sasa unaoanganza
kuanzia hapo Galilaya. Ni ukamilifu wa uaguzi wa nabii Isaya. Mpendwa msikilizaji
Yesu anachagua kuanzia utume wake hapa Kapernaum, mji mkuu wa Galilaya akiwa na lengo
maalumu kadiri ya mwinjili Matayo. Ni lengo gani hio?
Mpendwa, twatambua kuwa
watu wa Kapernaum walikuwa ni watu waliodharauliwa na watu wa Yerusalemu, walisadikika
kuwa watu wasiokuwa na akili na hata hawakuwa na uwezo wa kufuata sheria, wajinga
wa tamaduni zilizofundishwa na marabi. Kwa hakika Kapernaum ilikuwa na mchanganyiko
wa makabila tofautitofauti na hii ilikuwa ni sababu mojawapo ya dharau toka kwa Yerusalemu.
Bwana anaanza hapo utume wake hadharani akitaka kusema MWANGA SI TU KWA WALIOWAKAMILIFU
BALI HATA KWA WALE WALIOKUWA WAMETENGWA NA JAMII NA HAWA NDIO WA KWANZA KUSHUKIWA
NA MWANGA HUO. Mpendwa msikilizaji ili kuupokea mwanga huo ambao ni Kristu lazima
kuitikia agizo la Bwana na kadiri ya Matayo ni kutubu na kuamini kwa maana ufalme
wa Mungu umekaribia. Toba maana yake ni kubadilisha tabia, mwenendo na kuanza maisha
mapya, maisha yanayompendeza Mungu.
Mpendwa msikilizaji, kama tulivyoonesha
katika utangulizi sehemu ya II ya Injili inatupeleka kutafakari juu ya wito wa Mitume
ndiyo wito wetu hivi leo. Tunaona anawaita mitume 4 wa kwanza, na kwa hakika Matayo
hatuambii ni kwa namna gani aliwaita mitume hawa bali anataka kutuambia juu ya wito
wetu kama wakristu. Katika kuita Bwana inaonekana anaendelea na utume na safari, akitaka
kusema unapoitwa lazima kumfuata kwa haraka na kushughulikia mambo muhimu, si kusimama
wala kupumzika na kula na kunywa bali ni hekaheka za kitume katika familia na mahali
pote pa kazi.
Mtu anapoitwa kama tunavyoona wito wa hawa ndugu 4 anapaswa
kuitika chapuchapu pasipo kuchelewa! Katika kuwaita hawa ndugu wataalikwa kuacha wazazi
na kumfuata yeye. Hili laweza kuleta swali mbele yetu! Katika utamaduni wa kiyahudi
na hata wa kwetu hivi leo wazazi ndio wanaotuunganisha na mababu na mila za zamani
sasa iweje tuachane nao?
Mpendwa msikilizaji ni kweli wazazi wanalojukumu
hilo lakini si mila zote zinaendana na Injili, kumbe kuwaacha wazazi kwa Matayo ni
kuachana na mila zisizoendana na utamaduni wa MWANGA MPYA UTOKEAO PALE KATIKA MILIMA
YA GALILAYA! Mfano wa mila hizo ni kuoa wanawake zaidi ya mmoja, wivu, chuki, ushirikina,
uchawi na matunguli yanayozingira maisha na mioyo yetu.
Mpendwa msikilizaji,
mitume hawa watakuwa wavuvi wa watu, tofauti na kazi yao ya zamani ya kuvua samaki.
Ndiyo kusema watakuwa na wajibu wa kuwaondoa watu katika matatizo mbalimbali ambayo
yanawasilishwa kwa sura ya bahari. Kwa hakika bahari katika sehemu hiyo ya Injili
yataka kusema, machafuko, nguvu za giza, vita na mambo kama hayo.
Mfuasi wa
Kristo kamwe hataogopa kupambana na mizengwe kama hiyo, kwa maana anaongozwa na mwanga
tokea Galilaya. Haogopi kuongea na wavuta bangi, watumiao dawa za kulevya na wafanyao
mambo kinyume na maadili kulingana na mafundisho ya Kanisa. Mitume ni wale ambao hutenda
kazi ya kusaidia wagonjwa kiroho na kimwili wakiwagawia sakramenti za wokovu.
Mpendwa
mwana wa Mungu, nikutakie mwitiko daima katika maisha yako ukikumbuka ahadi zako za
ubatizo na ahadi nyinginezo katika maisha yako ya Kikristo. Tumsifu Yesu Kristo na
Maria Mama wa Mungu. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.