Mchakato wa kushirikishana imani Amerika ya Kusini
Kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani tarehe 25 na tarehe 26 Januari 2014, zitakuwa
ni siku maalum kwa ajili ya kukusanya mchango kwa ajili ya kuyasaidia Makanisa yaliyoko
Amerika ya Kusini katika maisha na utume wake.
Kampeni ya
Mwaka 2014 inaongozwa na kauli mbiu ”Kushirikishana Imani”. Baraza la Maaskofu Katoliki
Marekani, linatambua na kuthamini mchango na zawadi kubwa ya imani kutoka kwa waamini
wa Makanisa ya Amerika ya Kusini.
Ni mwaliko na changamoto ya kuhakikisha
kwamba, wanaendelea kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, tayari
kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika maisha ya kiroho na kiimani.
Wajitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea imani yao kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaendelea kusema kwamba, licha ya kuyapatia
msaada wa hali na mali, Makanisa ya Amerika ya Kusini, lakini Wamerikani wanayo mengi
ya kujifunza kutoka kwa Waamini wanaoishi huko Amerika ya Kusini.
Mchango
wa hali na mali kwa ajili ya Makanisa ya Amerika ya Kusini ulianzishwa kunako mwaka
1965, mara tu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tangu wakati
huo, imegota miaka 50 ya upendo na mshikamano kwa Waamini wa Makanisa ya Amerika ya
Kusini. Mchango huu unapania pamoja na mambo mengine kusaidia mwendelezo wa huduma
za kichungaji zinazotolewa katika nchi 25 zilizoko Amerika ya Kusini na Visiwa vya
Caribbiani.
Kipaumbele cha kwanza kinatolewa kwa miradi ya Uinjilishaji na
Katekesi, kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji Amerika ya Kusini.
Hii ni changamoto iliyotolewa na Maaskofu wa Amerika ya Kusini katika mkutano wao
maalum uliofanyika kunako Mwaka 2007 huko Aparecida. Waamini wote wanaalikwa na kuhimizwa
kuwa ni mashahidi na wamissionari kwa kutangaza Injili ya Furaha katika medani mbali
mbali za maisha.
Waamini watambue kwamba, kwa kutekeleza wajibu na dhamana
hii, wanashiriki kikamilifu katika utume wa Kanisa la Kiulimwengu, linalotumwa kutangaza
Injili hadi miisho ya dunia. Kwa miaka ya hivi karibuni, kiasi kikubwa cha mchango
uliotolewa, kilipelekwa kusaidia ujenzi wa Haiti mpya baada ya kukumbwa na tetemeko
la ardhi kunako mwaka 2010 na hivyo kusababisha maafa makubwa.