Mawasiliano lazima yaendeleze utamaduni wa kukutana
Alhamis, mjini Vatican, uliwasilishwa Ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya adhimisho
la 48 la Siku ya Mawasiliano Duniani, ambayo itakuwa tarehe Mosi June 2014. Ujumbe
wa Papa uko chini ya Mada, “ Mawasiliano katika huduma ya Utamaduni wa Kweli wa Kukutana”.Na
ulitolewa Alhamis kama sehemu ya kumbukumbu ya Maadhimisho ya Siku Kuu ya Msimamizi
wa Vyombo vya habari na wanahabari, Mtakatifu Francis de Sales, ambayo huadhimishwa
tarehe 24 Januari kila mwaka. . Papa Francisko katika ujumbe huu , anasisitiza
kwamba, si vyema kuwasilisha Injili kwa wengine iwapo sisi wenyewe mioyo yetu haiko
wazi katika maisha ya Kiinjili na katika kusikiliza ukweli wa wengine. Ujumbe huo
unasisitiza kwamba, kuwa shahidi wa kweli wa Kristu si uhodari wa kuwajaza watu na
maneno mengi ya kidini lakini hasa ni kujaribu kujibu maswali na mashaka yao, kwa
heshima na unyenyekevu katika maisha ya kiinjili. Askofu Mkuu Claudio Celli ,
Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mawasiliano ya Jamii, akiwasilisha ujumbe huo
kwa wanahabari, alitoa muhtasari kwamba, unjumbe wa Papa, una vipengere mbalimbali
vinavyogusa maisha ya kijamii kwa wakati huu , kuanzia utandawazi katika mawasiliano.
Unasisitiza vyombo vya habari na teknolojia ya mawasiliano ya kisasa, vitusaidie
kutukutanisha kwa ukaribu zaidi na kushirikishana mawazo kwa haraka hata na watu
wanaoishi katika maeneo ya ndani vijijini kusiko fikika kirahisi. Na kwamba utamaduni
wa kukutana unadai si tu kuwa watu wa kutoa lakini pia kupokea. Na pia mfumo wa utandawazi,uweze
kuhamasisha watu kukutana na kushirikishana na kujenga mshikamano. Papa ameeleza
kwa kutazama uwepo wa kashfa ya pengo kati ya utajiri wa matajiri na umaskini mkubwa
wa maskini, akionyesha tumaini lake kwamba, vyombo vya habari vinaweza kusaidia kutoa
kwa nguvu zaidi maana ya umoja wa familia ya kibinadamu .
Aidha Papa Francisko,
akiutazama upande wa pili wa mfumo huu wa mawasiliano ya haraka, ameonyesha kutambua
na kukubaliana kwamba kuna changamoto nyingi na halisi , kwa kuwa pia unaweza kujenga
utengano na uhasama kati ya watu kwa haraka sana. Lakini hili halihalalishi kupinga
maendeleo ya njia za mawasiliano, ila inakumbushwa kwamba, utalaam huu katika mawasiliano
si hatima ya binadamu lakini ni mafanikio tu katika teknolojia. Na hivyo Kanisani
lazima, liwe mfano katika matumizi mazuri ya nishati hii . Papa pia ametumia
mfano wa msamaria mwema, katika kuona umuhimu wa kuwa tayari kusaidia wengine, utayari
wa kuchukua jukumu la kubeba shida na mateso ya wengine. Na kwamba, katika mapinduzi
haya ya vyombo vya upashanaji habari na teknolojia ya habari, changamoto kubwa za
kusisimua, tunaweza kukabiliana nazo kwa nguvu mpya na mawazo mpya kwa njia ya
kushirikishana habari za uzuri wa Mungu na watu wengine.