2014-01-24 14:15:55

Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa!


Kardinali mteule Yeom Soo-Jung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, hivi karibuni alitembelea Kituo cha Caritas Korea kusalimia na kuzungumza na maskini pamoja na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kuwaonjesha upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Akiwa kituoni hapo, Kardinali mteule, ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hiki ni kituo ambacho kinahudumia watu wasiokuwa na makazi maalum wapatao 900, wengi wao ni wale ambao wameathirika kutokana na magonjwa mbali mbali.

Kardinali mteule amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteuwa kuwa ni kati ya washauri wake wa karibu katika maisha na utume wa Kanisa kama Kardinali na kwamba, baada ya kitambo si kirefu ataanza kuvaa mavazi ya rangi nyekundu, alama ushuhuda wa imani, hata kama ikibidi kuyamimina maisha kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Anasema hii ni dhamana nyeti kwa Makardinali wanaoalikwa kujisadaka kwa ajili ya Kristo. Amewaomba watu wanaotunzwa kituoni hapo kumsindikiza kwa njia ya sala katika utume wake ndani ya Kanisa la kiulimwengu. Amewakumbusha waamini hao kwamba, hata katika shida, mahangaiko na mateso yao, bado wanapendwa na Mwenyezi Mungu na Kanisa na kwamba, wanaendelea kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto ya kumwilisha na kushirikishana upendo huu na jirani wanaowazunguka.

Baada ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kardinali mteule alitembelea wagonjwa waliokuwa hawajiwezi na kusema kwamba, Kituo hiki kinapaswa kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa uwepo wa ufalme wa Mungu kati ya watu wake na kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni sehemu ya maisha na utume wa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul.

Watu wengi nchini Korea ya Kusini wanamkumbuka Kardinali mteule tangu alipokuwa Paroko, alionesha upendeleo wa pekee kwa maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kuanzisha kituo cha kuwapatia walau chakula kwa siku!







All the contents on this site are copyrighted ©.