Wakimbizi 26, 000 kurudishwa nchini Angola Mwaka 2014
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limeonesha mpangomkakati
wa kutaka kuwarudisha nchini mwao, wananchi 26, 000 kutoka Angola waliokua wamekimbilia
Zambia, Afrika ya Kusini, DRC na Bostwana ili kupata hifadhi wakati wa vita ya wenyewe
kwa wenyewe nchini Angola.
Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa
linaendelea kushirikiana na Serikali ya Angola ili kuweka mikakati makini kwa ajili
ya kuwapokea wananchi wa Angola wanaorudi nchini mwao baada ya amani na utulivu kuanza
kushika hatamu. Inakadiriwa kwamba, kila juma, zaidi ya wakimbizi 1, 200 watakuwa
wanarudishwa Angola katika eneo la Uige.
Umoja wa Mataifa unafafanua kwamba,
kwa wananchi wa Angola ambao wataridhia kubaki katika nchi zile ambazo ziliwapatia
hifadhi wakati wa vita wako huru na watapatia uraia na wale wanaorudi watafanya hivyo
kwa hiyari yao bila shuruti. Ufafanuzi huu umetolewa na Bwana Hans Lushof, Mwakilishi
wa UNHCR nchini Angola.
Takwimu zinaonesha kwamba, vita ya wenyewe kwa wenyewe
nchini Angola kuanzia Mwaka 1961 hadi mwaka 2002, ilipelekea watu zaidi ya millioni
nne kuikimbia Angola ili kuokoa maisha yao. Kuna wakimbizi laki sita wanaoendelea
kupata hifadhi katika nchi jirani na Angola.