2014-01-23 09:07:53

Umuhimu wa Muziki mtakatifu katika Liturujia ya Kanisa


Hivi karibuni Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliendesha semina maalum ya walimu wa nyimbo, Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na: Pd Paterni P. Mangi – Katibu Mtendaji Idara ya Liturujia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Uongozi wa Shikwaka Jimbo Kuu Dar es Salaam. Waalimu 108 wa kwaya kutoka katika Parokia za Jimbo Kuu la Dar e Salaam.
Ifuatayo ni tathmini ya Walimu wa Kwaya Jimbo Kuu la Dar es Salaam juu ya Kuuboresha Muziki Mtakatifu wa Kanisa Katoliki la Tanzania.
AGENDA
1. HALI YA MUZIKI WA KANISA KWA SASA
Katika kipindi cha miaka mitano hivi iliyopita muziki wa Kanisa umebadilika na umepitia katika mambo mengi sana baada ya kuibuka kwa vipaji vipya vya utunzi na upigaji kinanda. Hali hiyo imesababisha asili ya muziki wa Kanisa kwenda mrama na kutawaliwa sana na muziki wa mapambio; yaani watunzi wametoka kwenye mwelekeo na maelekezo ya Kanisa katika kutunga nyimbo.
2. KUHUISHA MUZIKI KATOLIKI TANZANIA
2.1 Mababa wa Kanisa Tanzania wamegundua hili na jitihada za makusudi zimeanza chini ya kitengo cha Liturujia TEC ngazi ya taifa ili kuunusuru muziki mtakatifu wa Kanisa Katoliki.
2.2 Hivi ili kurudisha hadhi ya muziki wa Kanisa na mwelekeo wa watunzi wetu, zinahitajika semina nyingi zaidi. Semina za walimu wa kwaya katika jimbo kuu la Dar es Salaam ziwe endelevu na zifanyike mara kwa mara ili walimu tutambue nafasi zetu na wajibu wetu katika Kanisa na jamii kwa ujumla.
2.3 Kuundwa kwa chombo maalumu ambacho kitafanya sensa ya nyimbo zote, na kwa kufuata vigezo vitakavyowekwa. Chombo hicho kipewe mamlaka ya kuziondoa nyimbo zisizofaa ili zisitumike katika ibada. Hii ni Kutokana na kuwepo kwa utitiri wa nyimbo nyingi kwa sasa. Azimio hilo baadaye lipewe baraka na kitengo cha liturujia ngazi ya taifa kwa utekelezaji wake.
3. UPATIKANAJI WA NYIMBO ZILIZOKWISHACHAPWA
Kutengenezwe tena vitabu vya nyimbo kama vile vya NL 1&2 vilivyotolewa
awali. Hata hivyo hatuna budi kujifunza na kutokurudia makosa ya matoleo ya
awali, kama vile:-
i. Toleo NL 1 lilikosewa sana kwani lilikusanya nyimbo za ukanda wa Kusini tu, pia majina ya watunzi wa nyimbo husika hayakuwekwa.
ii. Japo Toleo NL II lilikuwa na mabadiliko makubwa, katika matoleo yajayo inashauriwa yawe bora zaidi, kiusahihi wa kunakili nyimbo bila makosa na pia kwa kuwa makini na aina gani ya nyimbo zinawekwa. Kwa mfano unawekwa wimbo mpya wa “ Bwana ndiye mchungaji wangu”, ambao haujullikani kama ule wenye maneno kama hayo uliotungwa na mtunzi na gwiji la muziki Mwalimu John Mgandu.
iii. Baraza la Maaskofu kupitia kitengo chake cha liturujia kiwe na utaratibu mzuri wenye wigo mpana wa uwakilishi na ushirikishi wakati wa kuandika vitabu hivi.
4. UTAMADUNISHO WA SINODI YA AFRIKA
Dhana ya utamadunisho iliyotolewa katika Sinodi ya Afrika inahitajika kutafsiriwa upya kwa watu ili waelewe mipaka yake, kwani suala hili halijaeleweka kwa watu hadi sasa, wengi wakidhani kuwa utamadunisho ni kucheza Kanisani wakati wa kuimba!
5. WALIMU WA KWAYA – MAJUKUMU, MIPAKA NA SUALA LA ITHIBATI
5.1 Mipaka ya Utendaji kazi Walimu walio wengi hawajui mipaka yao katika utendaji wa kazi zao za kila siku za utume katika nyanja nyingi:-
5.1.1 Kiutawala: Wajibu wa walimu umeainishwa vema katika katiba za kwaya zao husika. Hivi mwalimu kuingilia suala jingine zaidi ya wajibu wake ni kuvuka mipaka na kuleta fujo katika vikundi.
5.1.2 Kiutunzi: Walimu wengi hubadilisha matini za nyimbo za liturujia (“matini” ni maneno ya nyimbo kadiri ya vifungu vya Biblia), na kuweka maneno yao ambayo si ya Biblia lakini pia yenye kuleta tafsiri potofu na tofauti na muziki mtakatifu wa Kanisa Katoliki. Kwa mfano maneno ya nyimbo / maneno kama vile:-
a. Mchanganyo Bwana Yesu amekataa,
b. Shetani kapata pancha safari haiendelei, na ule
c. Nimevunja mkataba na shetani
d. Kutumia maneno mepesi (circular words) kama vile “Yesu kavalishwa
nepi” badala ya “Yesu kavalishwa mavazi ya kitoto”

5.2 Walimu kukosa moyo wa ibada wawapo Kanisani. Walimu inabidiwafundishane kwa upendo elimu ya muziki badala ya kushindana bila sababu.
5.3 Upigaji wa kinanda:Wapigaji vinanda wameshindwa kutambua mipaka yao ya taalamu, mfano:-
5.3.1 Wapo wanaopiga chords tu kwa kukosa kufanya mazoezi ya nyimbo husika.
5.3.2 Wapo wanaotoa tuni ya wimbo mwingine, wakati wimbo utakaoimbwa ni mwingine.
5.3.3 Wapo wanaopiga tuni za nyimbo za mitaani (kwa mfano, Kamongo au mapambio ya ndoa) na tuni za nyimbo nyingine kwenye free organ ya wimbo husika wakati wa maadhimisho ya liturujia. Kimsingi hali hii inaonyesha ni namna gani wapiga vinanda walivyoishiwa kiutaalamu na hivi kuharibu uzuri wa muziki wa Kanisa Katoliki.
5.4 Wapo walimu wengi sana katika kwaya zetu ambao hutanguliza mbele matakwa yao wenyewe badala ya kufuata nini Kanisa linataka.
6 MAPAROKO NA VIONGOZI WALEI WA PAROKIA
6.1 Baadhi ya migogoro katika kwaya kwa kiasi kikubwa huchangiwa na maparoko na viongozi wa parokia zetu. Ni dhahiri kuwa wapo mapadre leo ambao tangu walipokuwa seminarini walikuwa hawapendi muziki, na kitu chochote wanachofanya wanakwaya, hata kama kiwe kizuri kinakuwa kosa. Imezoeleka sasa kuwa padre kuzuia kwaya isiimbe wimbo fulani au kuisimamisha kwaya isitoe huduma ni kitu cha kawaida.
6.2 Kitengo cha liturujia kiangalie namna ya kuweka utaratibu elekezi ambao utawasaidia maparoko kutoathiri utume wa uimbaji ambayo nao una nafasi kubwa sana katika kuihubiri Injili. Pamoja na changamoto hizi, walimu wa kwaya tuendelee kutumia busara kwa kupokea na
kurekebisha maagizo tunayopewa na hirakia za Kanisa mahalia.
6.3 Mapadre wanapaswa kuwaonyesha wanakwaya upendo kwani nao wanafanya kazi ya kuhubiri injili na kumsaidia padre katika maadhimisho ya misa. Pia mapadre wengi wanapenda kuendesha misa haraka haraka sana kama vile kuna kitu wanakimbilia baada ya misa. Hali hiyo inasababisha mapadre kuzuia kwaya isiimbe Bwana Utuhurumie na Utukufu hata siku za Jumapili (Solemnity) tena bila kufanya mawasiliano na kwaya hivi kuharibu uzuri (decorum) wa ibada.
Katika maisha ya sasa yenye changamoto kubwa za kiuchumi, wanakwaya hujitolea kwa moyo muda wao kwa ajili ya utume wa uimbaji hivyo Maparoko wanapaswa kuheshimu majitoleo hayo na hivyo kutoa ushirikiano na mawasiliano muafaka iwapo ratiba za ibada zinabadilika. Hii itafanya wanakwaya kutokuona wanapotezewa muda wao kwa mazoezi mengi walakini ibada inakatwakatwa sehemu za nyimbo.
6.4 Uelewa juu ya muziki wa Kanisa Katoliki usiishie tu kwa walimu bali ufikishwe pia kwa wanakwaya ili nao kama wadau waelewe maana yake na jinsi wanavyoweza kuutofautisha na miziki mingine.
7 TATIZO LA KIWANGO KIDOGO CHA ELIMU YA MUZIKI KWA WALIMU
7.1 Kurejea mada ya semina, mwalimu anatakiwa aweze kutofautisha kati ya muziki unaostahili kuimba Kanisani na ule wa mapambio unaostahili kuimbwa nje ya ibada na katika majukwaa. Ikitokea kuna mwalimu asiye na uelewa huo na akakutana na wanakwaya wenye uelewa kama wa kwake, muziki utakaoingizwa katika maadhimisho ya ibada utakuwa nje ya mwongozo wa ibada. Walimu wanatakiwa kujielimisha kwa kiwango kikubwa kimuziki na liturujia ili kuweza kuongoza kwaya.
7.2 Sio kila wimbo unaotungwa unaweza kukubalika. Watunzi wanaochipukia wajifunze toka kwa muziki uliotungwa na watunzi wa zamani (waliopumzika katika amani ya Bwana) kama vile: Padre Gregory Kayetta , Padre Daudi Ntampambata , Padre Stefano Mbuga , Felician Nyundo, John Mgandu, Joseph Makoye, Elias Kalluh, Joseph Mkomagu, Isaya Nganga Stansalus Mujwahuki, na wengine wengi.
7.3 Na pia kwa watunzi wasasa ambao muziki wao bado unatunza hadhi na maadili ya muziki wa Kanisa Katoliki kama vile: Padre Lui Mwanampepo, Charles Saasita, Venant Mabula, Beatus Idama, Dismas Mallya, Fortunatus Mallya, Faustine Mtegeta, Robert Kawite, David Wasonga, Benedict Simfukwe, n.k.
Kujifunza toka wanamuziki hawa itasaidia sana katika jitihada za kurudisha hadhi ya muziki wa Kanisa Katoliki Tanzania. Kikubwa hapa mwalimu anapaswa kuuvaa unyenyekevu kama wa Baba wa Kanisa Bonaventura aliyeichana kazi yake aliyoiandaa kabla hajaisoma kwa Baba Mtakatifu wa wakati ule, si kwa vile haikuwa na ubora bali kwa unyenyekevu aliheshimu kazi ya Thomas wa Akwino aliyoisoma mbele ya Baba Mtakatifu na ilikuwa na ubora mkubwa juu ya sifa za Ekaristi Takatifu. Unyenyekevu gani huu mkubwa ambao leo tunaweza kuuiga?
8 NINI KIFANYIKE SASA
8.1 Ni kazi kubwa sana kuurudisha ubora wa muziki wa Kanisa Katoliki. Ni wazi kuwa kwaya nyingi sasa zinaimba na kurekodi nyimbo za kisasa kutokana na soko lao la wakati huu lilivyo, na hii inatokana na wanamuziki wengi kuiga muziki wa dunia (taarabu, jazz, blues, sebene n.k) kinyume na muziki wa historia ya Kanisa (sacred and solemnal, liturgical). Hata Papa Pio X mwaka 1903 alitoa mwongozo juu ya muziki mtakatifu wa Kanisa Katoliki
(Tra le Sollecitudini Instaurare Omnia in Cristo). kwa lengo la kuurekebisha muziki wa Kanisa.
Hivyo kwa kuanzia:
8.1.1 Waamini waelimishwe juu ya mkakati huu wa kurudisha muziki wa Kanisa Katoliki.
8.1.2 Mapadre na maaskofu ambao baadhi yao ni mashabiki wakubwa wa miziki hiyo nao waelimishwe juu ya nia hii ya Kanisa.
8.1.3 Baraza la Maaskofu, chini ya kitengo chake cha liturujia lije na mikakati mahususi katika kutekeleza azma hii. Kwa mfano ni namna gani Kanisa litaufanya muziki wa kisasa kuwa na sura ya kikatoliki.
8.2 Ili kudhibiti ubora wa nyimbo, itengenezwe tovuti ya SHIKWAKA jimbo kuu la Dar es Salaam, ambapo marekebisho au ushauri utakuwa rahisi kutolewa.
8.3 Redio za Kanisa zitusaidie katika kuelezea uma juu ya nini maana ya muziki wa Kanisa Katoliki, na pia kwa kupiga katika redio hizo nyimbo zile za muziki wa Kanisa Katoliki.
9 MOYO WA KUJIFUNZA
Uwepo wa wana muziki wenye umri na ambao wamekuwa katika tasnia ya muziki wa Kanisa kwa siku nyingi walihudhuria semina hii. Hili ni jambo la kujifunza toka kwao hasa kwa wanamuziki wanaochipukia ambao wengi wao wanaona tayari wamefikia upeo katika muziki. Tumeona vema kutambua baadhi ya wanamuziki hao waliohudhuria semina hii ili tujifunze na kuongeza elimu ya muziki kutoka kwao katika tasnia hii ya muziki kwa ujumla. Hao ni kama:-
a. Benedict Simfukwe,
b. Robert Kawite,
c. Faustine Mtegeta,
d. Mwalimu Kanuti,
e. Justine Ncheye,
f. Fortunatus Mallya, na
g. Dismas Mallya.
Pia katika semina hii walihudhuria wataalamu wa muziki wa pekee (classics) ambao wanaendesha kikundi cha muziki kijulikanacho kama The Dar Choral Society. Muziki huu wa pekee (classical music) unahitaji nidhamu ya hali ya juu na moyo wa kujituma. Baadhi ya miziki inayopigwa na kikundi hiki huimbwa pia Kanisani nyakati za maadhimisho kama
Aleluya Kuu na miziki mingine
iliyotungwa na
George Frederick Haendel, Misa iliyotungwa na Wolfgang
Amadeus Mozart
, Johann Sebastian Bach, n.k. Wataalamu wa muziki huo
waliohudhuria semina hii ni:
a. Raymond Hekima, na
b. Paschal Mhangamkali Gunganamtwa
Kwa wanamuziki hawa licha ya uzuri wa kazi zao walizozitoa katika muziki bado wanaitikia kuja katika semina hizi na wamechangia mawazo katika kuboresha muziki wa Kanisa.
KINANDA
Kwa wapiga kinanda, ilishauriwa kuwa watenge muda wao wa kutosha kwa ajili ya kufanya mazoezi na si kufanya mazoezi wakati wa ibada. Tena watumie vitabu vya mwongozo ya majifunzo ya Kinanda, mf. Kitabu cha
Harmonium Schule kilichotungwa na Heinrich Bungart, na vitabu vingine kama hivyo, kwani kupiga Kinanda ni sanaa, na sanaa yoyote ili iwe nzuri ni lazima kujifunza na kufanya mazoezi mara kwa mara: Practice makes perfect.
10 Nyimbo za zamani na Gregorian chants
10.1 Hizi ni hazina ya Kanisa hivyo zinapaswa kufundishwa katika kwaya zetu. Yapo makanisa machache ambapo WIMBO WA KATIKATI una tuni moja tu inayotumika katika ibada zote mf. Parokia ya St. Peters, Oysterbay, hii inatoa ushiriki wa waamini wote kuimba kiitikio hicho.
10.2 Pia desturi ya kufundisha nyimbo za Kilatini katika kwaya zetu ni suala ambalo walimu inabidi tutilie mkazo ili ikiwezekana ndani ya mwezi kuwe na dominika moja ambayo nyimbo hasa Ordinarium (nyimbo zisizobadilika kila ibada) zitaimbwa kwa Kilatini.
11 UBORESHAJI WA NYIMBO ZA ZAMANI
11.1 Vipo vikundi vya muziki zikiwemo kwaya ambazo zinabadili nyimbo za zamani kwa kuweka vionjo vipya vya muziki kwa kuingiza midundo ya ngoma na hivi kuharibu uzuri wa awali wa wimbo husika. Hapa mfano umetolewa wa kikundi KAPOTIVE SINGERS, BUKOBA ambao wameubadili wimbo wa “ PENDO LAKO YESU LIMENIVUTIA NIWE WAKO MILELE ” na hivi kusikika tofauti kabisa na asili yake.
11.2 Pia zipo kwaya zinazoweka ngoma katika Gregorian chants. Kwa mfano, “Christus Vincit”, kitu ambacho hakikubaliki. Nyimbo hizi zinaimbwa bila ngoma.
12 MISALE YA KIRUMI
Utaratibu wa kufuata Misale ya Kirumi haujaeleweka na ipo haja ya kuwa na
mwongozo wa pamoja kwa parokia zote.
13 Idadi ya walimu wa kike katika semina walikuwa watatu tu kati ya walimu wa kiume 108 waliohudhuria. Akina dada na kina mama ambao ndio wanachukua asilimia kubwa sana katika kwaya zetu wahamasishwe katika kujifunza muziki.
MAAZIMIO:
1. Semina nyingine ambayo itakuwa ya ukubwa zaidi itafanyika kabla ya kuanza kwa Kwaresma na itahusisha:
a. Masomo juu ya nadharia ya sheria za utunzi, harmony n.k
b. Uimbishaji wa kwaya (Conducting patterns)
c. Upigaji wa Kinanda (Keyboard playing)
2. Semina hizi pia zipelekwe kwenye majimbo mengine.
3. Miongozo ya sheria zinazotakiwa katika utunzi wa muziki mtakatifu wa Kanisa Katoliki zitatolewa kwa walimu
4. Tathmini ya walimu itatolewa katika magazeti ya Kanisa Katoliki na kutangazwa katika redio za Kanisa katika vipindi maalumu.
5. Kuundwa kwa kamati maalum za kiliturujia zikijumuisha walimu.
6. Kwaya zirudishe desturi ya kutunga nyimbo za kiliturujia: Misa, Zaburi, Sadaka, Komunio, Shukrani, Tafakari n.k. badala ya kuimba nyimbo za mapambio ili kuivutia hadhira. Tena uzoefu unaonyesha kuwa walimu wengi wa kwaya huwa wanawafundisha nyimbo wanakwaya kwa ajili ya kurekodi hivyo mwanakwaya hukosa nafasi ya kuhoji aina ya nyimbo wanazofundishwa.
UCHUNGUZI KIFANI (CASE STUDY)
Kuna kwaya ilienda kurekodi katika studio ambapo wataalamu wa kurekodi, “sound engineers” ni wakristo wa madhehebu yasiyo ya Kikatoliki. Baada ya kurekodi nyimbo na wakiwa wanaelekea kumaliza kurekodi walirekodi wimbo wa marehemu Nganga wa, “Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote…”, wale wataalamu wakasema kwa mshangao, “Loo! Hatimaye kwaya hii sasa imerekodi wimbo wa Kikatoliki!” Kuacha desturi ya kuimba nyimbo za Kanisa Katoliki hushtua hata watu wengine na si Kanisa Katoliki tu. Kumbe ni vizuri kubaki katika reli kama alivyoshauri mwanamuziki mmoja mkongwe.
Hivyo basi:-
1. Ithibati: Nyimbo za kurekodiwa zipitishwe kwa kamati ya liturujia jimbo ili kupata kibali. Hata kama padre mhusika hajui muziki lakini atasaidia katika kushauri juu ya maneno yaliyotumika yasije yakaleta mafundisho ya kukufuru (profanity).
2. Katika kujifunza jinsi kazi za muziki zilivyo, walimu wapate muda wa kuhudhuria “concerts” ambazo mwalimu Raymond Hekima anaziandaa. Kuna mengi mazuri ya kimuziki yatapatikana.
3. Katika hatua za kurudisha tungo za muziki wa Kanisa Katoliki, zinakusanywa nyimbo za wanamuziki waliotutangulia mbele ya Bwana kama vile: Felician Nyundo, John Mgandu, Joseph Makoye, Elias Kalluh, Joseph Mkomagu, Isaya Nganga, Stansalus Mujwahuki, Antony Sing’ombe, Guido Matui na wengine na kutengeneza vitabu vya nyimbo zao.
HITIMISHO
Muziki mtakatifu wa Kanisa Katoliki ulioharibiwa utarudishwa na walimu wa kwaya kwa ujumla. Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia ngazi ya Taifa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Fadre Paterni Mangi anatambua kuwa asilimia kubwa ya muziki wetu umeharibika na ana nafasi kubwa ya kurudisha hadhi yake na ametangaza kuwa safari ya kuurudisha muziki wa Kanisa Katoliki imeanza sasa na anaomba tushirikiane sote katika kurejesha hadhi ya muziki wa Kanisa Katoliki.
Imeandikwa na:-
1. Francis Mhagama, na
2. Justine Ncheye
Na kuhakikiwa na:-
Pd. Paterni P. Mangi - Katibu Mtendaji Idara ya Liturujia – TEC
03.12.2013
DAR ES SALAAM








All the contents on this site are copyrighted ©.