Papa Francisko anafuatilia kwa makini na masikitiko makubwa yale yanayoendelea kutendeka
Sudan ya Kusini
Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican Sudan ya Kusini anasema, Baba
Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa makini machafuko ya kisiasa nchini Sudan
ya Kusini yaliyopelekea watu wengi kupoteza maisha na wengine kuyakimbia makazi yao
kwa kuhofia usalama wao. Anawaalika viongozi wa Serikali na Kisiasa kuweka silaha
chini na kuanza mchakato wa majadiliano yanayopania upatikanaji wa amani ya kudumu.
Askofu
mkuu Balvo ameyasema hayo mapema juma hili, alipowasili mjini Juba ili kushiriki katika
mkutano maalum wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini, unaoendelea
hadi tarehe 30 Januari 2014. Askofu mkuu Balvo anawaalika vijana na wananchi wenye
mapenzi mema Sudan ya Kusini, kujikita katika amani na mapatano ili kuondokana na
falsafa ya vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa katika Jamii.
Askofu
mkuu Balvo anawapongeza Maaskofu kwa kuendelea kushikamana na kujitoa kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan katika ujumla wake. Anawaalika viongozi wa
Kanisa kuwa kweli ni mashahidi wa Injili ya Kristo hata katika mazingira magumu kama
yanavyojionesha nchini Sudan ya Kusini.
Neno la Mungu ni ujumbe wa matumaini
na mapendo, unaojikita katika imani, ujasiri na nguvu, changamoto kwa Maaskofu kuwashirikisha
Wakristo wao Injili ya Furaha na Amani, kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili.