2014-01-22 11:05:06

Ujumbe wa Papa Francisko kwa kongamano la kiuchumi- Davos


Baba Mtakatifu Francisko akijali kila hali ya maisha ya watu duniani, alituma ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la Kiuchumi la Duniani, lililofunguliwa katika mji wa mapumziko wa Davos Uswiss, jioni ya Jumanne 21 Januari 2014. Ujumbe wa Papa ulitumwa kwa Profesa Klaus Schwab, Mwenyekiti Mtendaji wa Kongamnao la Uchumi Duniani.

Viongozi wa Kanisa Katoliki ni miongoni mwa wale wanaoshiriki katika kongamano hili la siku nne , ambalo linaongozwa na kauli mbiu ” Mfumo mpya wa dunia : Matokeo yake kwa jamii, Siasa na Biashara. Katika ujumbe huu, Papa Francisko anasema ni muhimu kusifu hatua zinazochukuliwa kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya watu katika maeneo ya afya, elimu na mawasiliano na kutambua jukumu la msingi kwamba, utendaji wa sasa katika biashara unatakiwa kuleta mabadiliko chanya.

Hata hivyo, anasema, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana, kwa bahati mbaya, yameongeza kusababisha kuenea kwa jamii kutengana, na hasa mpanuko wa pengo, kati ya maskini na matajiri, waume kwa wake ambao bado wanateswa na madhara ya ukosefu wa usalama kila siku.

Papa Francisko amesisitiza, jukumu muhimu kwa wanasiasa na wachumi, ni kukuza mbinu za utendaji zenye kujenga ushirikiano na umoja, ambamo utu wa kila binadamu na manufaa ya wote huzingatiwa.
Anasema suala hili, ni lazima liwe msingi wa kufanya maamuzi ya kila mfumo wa kisiasa na kiuchumi, ambalo mara nyingi hupewa uzito kidogo. Papa ameeleza na kukumbusha pia kwamba, wale wanaofanya kazi katika sekta hizi, wana wajibu nyeti kwa maisha ya wengine, hasa watu dhaifu zaidi na wanaoishi katika mazingira magumu.

Papa anasema, kwa watu wenye mapenzi mema, ni ngumu kuvumilia kuona kwamba, maelfu ya watu wanaendelea kufariki dunia kila siku kutokana na njaa , ingawa dunia ina chakula cha kutosha ambacho huharibika bure. Na pia si rahisi kuacha kujali hali ya wakimbizi wanaotafuta kuboresha maisha yao, hasa wale wanaopambanishwa na hali ngumu katika nchi mpya wanazo ingia wale wanao ishia kuangamia.


Papa Francisko amemalizia ujumbe wake kwa kutaja kinachohitajika kwa sasa , ni uwepo wa mwono mpya, uwazi na kupanua zaidi hisia za uwajibikaji kwa wahusika wote, unaoweza kuongoza shughuli za kiuchumi na fedha kwa uadilifu na utu zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.