Msiogope! Ishuhudieni imani kwa ujasiri! Uwepo wenu Zanzibar si ajali!
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea hotuba ya Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka 150 ya Uinjilishaji endelevu Jimbo Katoliki Zanzibar, Jumapili tarehe 19
Januari 2014 iliyosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu
Katoliki Arusha.
Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Kardinali Polycarp Pengo,
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Zanzibar
imetakiwa kufanya tafakari kwa kujiuliza ni kitu gani kilichofifisha imani wakati
fulani Visiwani hapo?
Sasa unaweza kujitajirisha mwenyewe!
Mwadhama
Polycap Kardinali Pengo, Mh. Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein, Mhashamu Askofu
Augustine Shao, Wahashamu Maaskofu Wakuu, Wahashamu Maaskofu, Waheshimiwa
Mapadre, Watawa na Taifa la Mungu,
“Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana, Tufurahi
na kuishangilia!”
Wapendwa Taifa la Mungu, leo tunayo kila sababu ya kufurahi,
kushangilia, na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani kwa Mungu katika Kanisa, ambayo
kwayo leo tunakusanyika hapa. Leo tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 150 ya Ukristo
ulioendelevu na wakudumu hapa Zanzibar tuliopokea toka wamisionari walipoingia kwa
mara nyingine tena mwaka 1863, safari hii wakitokea Jimbo la St. Denis, Reunion. Hiki
ni kipindi endelevu na cha kudumu kwani hapo kabla ukatoliki ulishafika Zanzibar wakati
wamisionari kutoka Ureno walipofika hapa mwaka 1498. Ukristo ulidumu kwa karne mbili
kabla ya Wamisionari kufukuzwa na Waarabu mnamo mwaka 1698.
Tunakusanyika hapa
leo kwa wingi wetu kumshukuru Mungu kwa sababu Jimbo la Zanzibar litabaki kuwa “Jimbo
mama yetu wa Imani”, kwa sababu ni kupitia mlango wa Zanzibar imani Katoliki ilitufikia
Tanzania Bara na maeneo mengine ya Afrika Mashariki na Kati. Mbegu ile ya imani iliyopandwa
Zanzibar imekua na kuwa mti mkubwa unaoendelea kukua na kuzaa matunda ya kudumu katika
imani. Kwa hiyo, pamoja na kumshukuru Mungu, tumekuja hapa tena kusali pamoja na kumuomba
Mungu atujalie neema na ujasiri wa kuwa Wamisionari imara na jasiri wa “Uinjilishaji
wa kina ulio endelevu na wa kudumu”.
Wapendwa Taifa la Mungu; pamoja na furaha
tunayokuwa nayo leo, tunatambua pia kuwa Kanisa la Zanzibar, katika ujumla wake, linapita
katika kipindi cha misukosuko ya kiimani. Matukio ya hivi karibuni ya mashambulizi
ya chinichini na hata ya waziwazi, mauaji ya viongozi wa dini ya kikristo n.k yanachora
picha ya kukosekana uhuru wa kuabudu na kuheshimiana. Kwa msisitizo mkubwa, tunapenda
kutoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kulinda na kutetea haki za watu wote
katika Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Tanzania ni nchi yenye watu wenye makabila
tofauti, dini tofauti na hata madhehebu tofauti. Hakuna Mtanzania aliyemkimbizi ndani
ya Tanzania. Mkristo anayeishi Zanzibar, kama alivyo mtu wa dini nyingine yoyote ana
haki sawa kikatiba. Tofauti zetu, ili mradi hatuvunji sheria, ndio utajiri wetu. Utofauti
wetu ndio unaotufanya tukamilishane. Hivyo, tunaomba serikali na watu wote wa Zanzibar
tuwe waamini wa msingi wa kwanza kabisa wa maisha ya mwanadamu kuwa: “sote ni wana
wa Mungu, kabla ya dini zetu, rangi zetu, makabila yetu.” Wito wetu si kwamba tuvumiliane
bali tuheshimiane, tupendane na tudumishe umoja wetu.
Wapendwa Taifa la Mungu,
tunapenda leo kutoa shukrani zetu na pongezi za dhati kwa Mhashamu Baba Askofu Augustino
Shao kwa utume uliotukuka. Tunapenda kukupongeza wewe Baba Askofu, Mapadre, Watawa
na Waamini wote kwa ujasiri wenu, moyo wenu wa kujitolea mkimhudumia kila mtu bila
kujali dini yake, kabila lake, wala rangi yake.
Huo ndiyo ukristo. Hiyo ndiyo
fahari ya imani tunayoitangaza; yaani kuiona sura na mfano wa Mungu katika kila mtu
aliyeumbwa na Mungu. Ushuhuda wenu wa imani unatuimarisha sote, hivi kwamba leo tunakuja
hapa kusema: “asante sana,” na “tuko pamoja nanyi.”
Wapendwa wanakanisa la
Zanzibar, ninyi si kanisa dogo: “Usiseme mimi ni mtoto; kwa sababu kokote nitakako
kutuma utakwenda” (Yer 1:7). Hivyo ndivyo Bwana anavyomwimarisha nabii. Ninyi si wadogo.
Mama hawezi kuwa mdogo. Ninyi Kanisa la Zanzibar ndiyo mliotumwa kuisambaza imani
Afrika Mashariki na Kati na bado mnayo dhima kuwa ya ushuhuda.
Msiogope! Ishuhudieni
imani kwa ujasiri! Uwepo wenu Zanzibar si ajali bali ni mapenzi ya Mungu. Mchango
wenu katika maendeleo ya Zanzibar katika nyanja za elimu, afya, utamaduni, n.k., ni
mkubwa sana. Tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada za kulinda
watu wote na Kanisa linazidi kuomba ushirikiano zaidi katika kutimiza majukumu mbalimbali
ya kidini pamoja na ya kijamii.
Baba Askofu na wanakanisa wa Zanzibar tunarudia
kusema Msiogope! Hilo ni himizo la Kristo Mfufuka aliyeshinda mauti na kifo. Simameni
imara katika Imani, simameni imara katika ukristo, simameni imara katika kukuza tunu
zetu kama Taifa la Mungu. Amina.