Mshikamano wa dhati na wananchi wa Sudan ya Kusini
Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini, Jumanne tarehe 21 Januari
2014 limeanza mkutano wake wa dharura unaotarajiwa kukamilishwa hapo tarehe 30 Januari
2014 kwa kutoa tamko rasmi la Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan kuhusu kinzani na
vita inayoendelea nchini Sudan ya Kusini.
Mkutano wa Maaskofu unafanyika wakati
muafaka ambapo wananchi wa Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini wanakabiliana na hali ngumu
ya maisha kutokana na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kusababisha maafa makubwa
kwa watu na mali zao.
Baadhi ya hati za kusafiria za viongozi wa Kanisa kutoka
Sudan kongwe zinashikiliwa na vikosi vya ulinzi na usalama kiasi kwamba, wameshindwa
kuhudhuria mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini.
Safari ya kikazi iliyofanywa na Askofu mkuu Charles Daniel Balvo Balozi wa
Vatican nchini Sudan ya Kusini imeonesha moyo wa mshikamano na wananchi wa Sudan ya
Kusini kutoka kwa Mwakilishi wa Baba Mtakatifu.
Licha ya majanga yanayoendelea
kujitokeza Sudan ya Kusini, lakini bado waamini wanaendelea kuishuhudia imani yao
kwa ujasiri, furaha pamoja na mshikamano kwa njia ya sala.