2014-01-22 10:18:27

Mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini duniani ni kati ya mambo yanayowagusa Papa Francisko na Rais Barack Obama!


Rais Barack Obama wa Marekani wakati wa ziara yake Barani Ulaya, itakayofanyika mwezi Machi 2014 atatembelea Uholanzi, Ubelgiji na Italia. Akiwa nchini Italia, Rais Obama atakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Rais Giorgio Napolitano wa Italia. Akiwa nchini Uholanzi kuanzia tarehe 24- 25 Machi, Rais Obama atashiriki kwenye mkutano mkuu juu ya Usalama wa nguvu za Nyuklia, ambao umeandaliwa na Serikali ya Uholanzi kwa kuwashirikisha viongozi kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.

Lengo la mkutano huu ni kuweka mbinu mkakati wa kudhibiti silaha za kinyuklia ili zisijekutumbukia katika mikono ya magaidi na hivyo kusababisha majanga kimataifa. Rais Obama atakuwa pia na mazungumzo na viongozi wakuu wa Serikali ya Uholanzi.

Tarehe 26 Machi 2014, Rais Obama ataelekea Brussels, Ubelgiji kuhudhuria mkutano kati ya Serikali ya Marekani na Viongozi wa Umoja wa Ulaya. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Obama kutembelea Makao makuu ya Umoja wa Ulaya. Atafanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Ubelgiji pamoja na Katibu mkuu wa NATO.

Kilele cha ziara ya Rais Obama ni hapo tarehe 27 Machi 2014 atakapokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani zinaonesha kwamba, Rais Obama anatarajia kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko mikakati na sera zake za kiuchumi katika mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato; mambo ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika utawala wa Rais Obama. Anatambua kwamba, mapambano dhidi ya umaskini duniani ni changamoto ya kimaadili miongoni mwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa.

Rais Obama, Julai 2009 alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Vatican ilionesha msimamo wake unaopinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba pamoja na kifo laini. Kanisa linapinga pia matumizi ya viinitete katika tafiti za kimaabara, kwani jambo hili linadhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameendelea kukazia msimamo na Mafundisho ya Kanisa kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na kwamba, wazazi na walezi wanalo jukumu la kuwalea watoto wao kiroho na kimwili.

Mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini duniani ni kati ya ajenda zinazopewa msukumo wa pekee na viongozi mbali mbali wa dunia hasa kutokana na madhara makubwa yaliyosababishwa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.