Licha ya majanga, kinzani na misigano mbali mbali, Nigeria itaendelea kushikamana
kama taifa moja!
Mwaka 2014 ni muhimu sana kwa historia ya wananchi wa Nigeria, kwani wanaadhimisha
Jubilee ya Miaka 100 ya Umoja wa Kitaifa baada ya kuunganisha Falme za Kaskazini na
Kusini na hivyo Nigeria kama inavyojulikana kwa sasa ikaundwa.
Licha ya majanga,
kinzani na misigano mbali mbali ya kisiasa, kijamii na kiimani inayoendelea kujitokeza
nchini Nigeria, lakini bado Nigeria kama taifa litaendelea kuwepo na kwamba, Mwenyezi
Mungu hatawaacha watu wake wagawanyike tena! Dhana hii inapaswa kufanyiwa kazi na
wanasiasa kwa kuonesha utashi wa kisiasa unaopania kujenga na kudumisha msingi wa
umoja na mshikamano wa kitaifa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu Josiah
Idowu Fearon wa Kanisa Anglikani, Jimbo la Kaduna, nchini Nigeria, wakati huu Nigeria
inapojiandaa kuadhimisha kilele cha Jubilee ya Miaka 100 ya Umoja wa Kitaifa sanjari
na maandalizi ya uchaguzi mkuu hapo mwakani. Umoja wa Kitaifa nchini Nigeria unajikita
katika imani kwa Mungu mmoja ingawa wakati mwingine kuna misigano katika uelewa huu
kiasi cha kusababisha mauaji na hata vita vya kidini, dhana ambayo kwa sasa imepitwa
na wakati.
Ni matumaini ya Askofu Fearon kwamba, hata baada ya uchaguzi mkuu
nchini Nigeria, unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015, Wananchi wa Nigeria ambao wengi
wao ni Wakristo na Waislam wataendelea bado kushikamana, kwani kuna kikundi cha watu
wachache wanaotaka kuivuruga nchi kwa mafao yao binafsi, wakati mwingine kwa kutumia
mgongo wa masuala ya kidini, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi, umoja na mshikamano
wa kitaifa.
Askofu Fearon anawaalika viongozi nchini Nigeria kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa heshima na utu wa binadamu; maendeleo na mafao ya wengi na kamwe wasitafute
nafasi za uongozi kwa ajili ya kujineemesha wao na familia zao. Viongozi wawe mfano
wa kuigwa; wanaosimama kidete kulinda na kutetea umoja na mshikamano wa kitaifa; ukweli
na uhuru wa wote bila kumezwa na udini pamoja na ukabila mambo ambayo ni sumu ya umoja
na mshikamano wa kitafa.
Serikali iwe makini kuwalinda watu na mali zao, ili
kudhibiti vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa ni tishio kwa usalama wa wananchi na
mali zao nchini Nigeria, hali ambayo imewafanya baadhi ya wananchi wenye uwezo kukodi
walinzi wa kujitegemea.