2014-01-21 08:38:25

Mashemasi ni wahudumu wa Injili, changamoto ya kujisadaka kweli kweli!


Daraja ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo kwa mitume huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati: hivyo hiyo ni Sakramenti ya huduma ya kitume. Ina ngazi tatu: Ushemasi, Upadre na Uaskofu. Hayo yamesemwa na Askofu mstaafu Paolo Nicolo' wakati alipokuwa anatoa Daraja la Ushemasi kwa Mafrateri wa Shirika la Mapendo, maarufu kama Warosmini: Richard Munyao Mwanzia kutoka Jimbo Katoliki la Machakosi, Kenya na Fulgence Oisso Epimaki kutoka Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania.

Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa kuu la San Giovanni a Porta Latina, lililoko mjini Roma, Jumapili tarehe 19 Januari 2014 na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Mapadre, Watawa na Waamini walei kutoka Afrika ya Mashariki, ili kushuhudia Maftraeri hawa wakipewa Daraja la huduma ndani ya Kanisa.

Askofu mstaafu Paolo Nicolo' anasema, Kristo ambaye Baba alimtakasa na akamtuma ulimwenguni, kwa njia ya mitume amewafanya mahalifa wao, yaani Maaskofu, wawe washiriki wa utakaso wake na utume wake. Na Maaskofu hawa kwa zamu yao, wamekabidhi kihalali kazi ya huduma yao kwa washiriki mbali mbali wa Kanisa na kwa ngazi mbali mbali. Kazi yao ya huduma imetolewa na Mapadre na Mashemasi ambao kwa njia ya Daraja Takatifu hupokea Mpako wa Roho Mtakatifu na kupigwa chapa kwa alama ya pekee inayowafananisha na Kristo kuhani mkuu ili waweze kutenda kwa jina na kwa nafsi ya Kristo, kichwa cha Kanisa.

Askofu mstaafu Nicolo' anasema, Mapadre ni washiriki wenye hekima wa daraja ya Uaskofu na wanaitwa kulihudumia Taifa la Mungu, kwani Mapadre huunda pamoja na Askofu wao ukuhani mmoja kwa kazi mbali mbali. Kimsingi wao ni wahudumu wa Sakramenti ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Upatanisho, unaowakirimia waamini huruma na upendo wa Mungu.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo kwa kupewa chapa isiyofutika na hufananishwa na Kristo aliyejifanya "Shemasi" yaani Mtumishi wa wote. Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Askofu na Mapadre katika Maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu, hasa Ekaristi Takatifu; kugawa Komunyo Takatifu, Kusimamia na kubariki ndoa; Kutangaza na kuhubiri Injili; kuongoza mazishi na kujitoa kwa huduma mbali mbali za mapendo, hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Askofu mstaafu Nicolo' anasema huduma ya mapendo kwa maskini inahitaji moyo wa kujisadaka; majiundo na malezi makini: kiroho na kimwili, kwa kutambua changamoto zilizoko pamoja na kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Mashemasi wanachangamotishwa na Mama Kanisa kudumisha maisha ya useja kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na kwamba, useja ni zawadi inayokabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi, kumbe, ni jukumu la Shemasi Richard Mwanzia Munyao na Fulgence Oisso Epimaki, kuendelea kujikita katika maisha ya useja, kielelezo cha uaminifu na utakatifu wa maisha kwa kumfuasa Kristo aliyekuwa: fukara, mtii na mseja. Useja ni mwaliko wa ushuhuda wa huduma kwa Mungu na Kanisa.

Mashemasi wamekumbushwa umuhimu wa kujikita katika maisha ya Sala kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu na kwamba, kwa njia ya Daraja la Ushemasi sasa wanawajibika kusali Sala ya Kanisa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya Taifa la Mungu. Huu ni wajibu wa kimaadili kwani maisha ya Kikuhani hayana budi kujengeka katika msingi wa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya Huruma hasa kwa Wanashirika la Mapendo, maarufu kama Warosmini.

Askofu Paolo Nicolo' ambaye mahubiri yake yalikuwa kama Katekesi endelevu kwa umati mkubwa wa Mapadre na Watawa kutoka Afrika Mashariki, aliwataka Mashemasi kuwa mstari wa mbele kuwasaidia waamini wanaoyumba yumba, kuwa makini kwa njia ya majadiliano binafsi, kwa kutumia njia za mawasiliano ya kisasa lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye harufu nzuri. Mashemasi watekeleze wajibu na dhamana yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya furaha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na kamwe wasimezwe na malimwengu, huko watakiona cha mtema kuni!

Makleri kwa ujumla wao, wawe ni mashahidi amini wa Injili, hekima na fadhila za Kimungu na kwamba, Ushemasi ni huduma endelevu ndani ya Kanisa inayorutubishwa kwa maisha ya Kijumuiya. Mashemasi wapya wajitahidi kujenga umoja na mshikamano wa upendo kama alivyofanya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Mashemasi waoneshe utii kwa Kanisa na Viongozi wao wa Shirika. Mashemasi wapya walikabidhiwa pia Zana za Kazi, yaani Injili wanayopaswa kuiamini na kuitangaza; kuifundisha na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.