Vita na kinzani za kijamii vinaangamiza maisha ya watoto wengi Barani Afrika
Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao
ya kijamii alisema kwamba, vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia inaangamiza
maisha ya watoto wengi. Hawa ni watoto ambao wamepokonywa zawadi ya maisha ya utotoni.
Mustakabali wa watoto wengi Barani Afrika hasa katika Nchi kama Sudan ya Kusini,
Jamhuri ya Afrika ya kati, DRC na kwingineko uko mashakani. Angalisho hili limetolewa
hivi karibuni na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF. Watoto ndio
wanaoendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa na vita inayoendelea huko Sudan ya Kusini.
Inakadiriwa kwamba kuna zaidi ya watu 400, 000 hawana makazi maalum nchini humo na
kuna idadi kubwa ya watu wanaendelea kufariki dunia.
Katika siku za hivi karibuni
zaidi ya watu, 200, 000 wamekimbilia kwenye Kambi za Wakimbizi zinazosimamiwa na Shirika
la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Mwakilishi wa UNICEF Barani Afrika Bwana
Lyorlumun Uhaa anasema, kamwe watoto wasihusishwe kwenye mgogoro wa kivita na kama
ikitokea hali kama hii vyama husika viwajibishwe kisheria.
Hivi karibuni watoto
wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 waliokuwa wametekwa nyara na kikundi cha watu
wenye silaha Mjini Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, wameachiwa huru baada
ya mazungumzo mazito kati ya Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Serikali ya Mpito.
Watoto hao kwa sasa wanahudumiwa kwenye Kambi zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa na
wamepewa fursa ya kuendelea na masomo yao wakati ambapo mipango ya kuwarudisha kwenye
familia zao inaendelea kufanyika.
Ukosefu wa ulinzi na usalama katika baadhi
ya maeneo kunahatarisha maisha ya watoto wengi katika maeneo yenye vita na kinzani
za kijamii, anasema Souleymane Diabatè, Mwakilishi wa UNICEF, Jamhuri ya watu wa Afrika
ya Kati.