Uchu wa mali na madaraka visilitumbukize taifa katika vita na majanga!
Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini linawataka wahusika wakuu katika vita ya wenyewe
kwa wenyewe inayoendelea kusababisha majanga makubwa nchini humo kusitisha mara moja
vita hiyo bila masharti na kuendelea kujikita katika majadiliano yanayopania kupata
suluhu ya amani na maendeleo ya kweli nchini humo.
Uchu wa madaraka unataka
kulitumbukiza taifa katika maafa ambayo yatakwamisha hata kiwango kidogo cha maendeleo
kilichoanza kupatikana tangu Sudan ya Kusini ilipoamua kuwa ni nchi huru.
Viongozi
wa Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini, wanawataka wahusika wote kuondokana na falsafa
ya kutumia nguvu kufikia malengo yao ya kisiasa na badala yake wajikite katika majadiliano
yanayosimikwa kwenye misingi ya ukweli na uwazi. Kila mwananchi anawajibu wa kulinda
na kutetea umoja na mshikamano wa kitaifa ambao umepitia katika magumu. Mwaka 2010,
kwa pamoja walijiunga na kupiga kura ya maoni na tarehe 9 Julai 2011 wakasherehekea
Uhuru wa Sudan ya Kusini.
Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, baada ya miaka
miwili tu ya Uhuru, wananchi wa Sudan ya Kusini wameanza tena vita ya wenyewe kwa
wenyewe! Kuna maelfu ya watu ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia
usalama wa mali na maisha yao.
Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini katika ujumbe
wake linasema: watu wametenda dhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze
kujipatanisha na jirani zao, kama sehemu ya mchakato wa uponyaji. Wananchi wajikite
katika amani badala ya kuvumisha mambo yanayowagawa na kuwasambaratisha kama nchi
moja. Wanasiasa waendeleze majadiliano ya kweli kwa ajili ya mafao na ustawi wa wananchi
wote wa Sudan ya Kusini.
Wananchi wote wasimame kidete kulinda na kutetea
zawadi ya maisha, wakate kujitumbukiza katika vita. Watu ambao wamevunja Katiba ya
nchi wafikishwe kwenye mkondo wa sheria na kamwe watu wasijichukulie sheria mikononi
mwao. Serikali na wapinzani watoe nafasi kwa Mashirika ya Misaada kutoa huduma kwa
wananchi na kwamba, umefika wakati wa kujikita katika mchakato wa amani.
Viongozi
wa Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini wanaipongeza IGAD na Jumuiya ya Kimataifa kwa
kuendelea kutoa misaada pamoja na kuhamasisha majadiliano ya kisiasa ili amani ya
kweli iweze kupatikana nchini Sudan ya Kusini. Wanayapongeza Makanisa kwa kuendelea
kutoa huduma kwa watu wanaohitaji msaada. Wataendelea kuhamasisha amani, ukweli, msamaha
na upatanisho, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa. Wanawataka wananchi wasikubali
kugawanywa kwa misingi ya kisiasa, kidini wala kikabila. Kila mwananchi awajibike
katika kujenga nchi yake na kamwe asiwe ni sababu ya kubomoka na kuporomoka kwa maendeleo
yaliyofikiwa hadi sasa.