2014-01-18 10:39:38

Viongozi wa Expo 2015 Milano wakutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014 amekutana na Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano pamoja na ujumbe wake kutoka Milano wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya Onesho la Expo Milano kwa Mwaka 2015. Katika mazungumzo yao, viongozi kutoka Milano wamemwalika Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika Onesho hili la Kimataifa litakalozinduliwa hapo tarehe Mosi, Mei 2015 na kufungwa rasmi tarehe 31 Oktoba 2015.

Onesho hili linaongozwa na kauli mbiu "Kulisha ulimwengu, nishati kwa ajili ya maisha". Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na Kardinali Angelo Scola wamefafanua kanuni msingi zinazopaswa kufuatwa na Mashirika ya Kanisa Katoliki katika kushiriki onesho hili la kimataifa. Baba Mtakatifu ameonesha kuvutiwa na mwaliko huo na kuwataka wahusika wakuu kuhakikisha kwamba, wanamwilisha moyo na ari ya huduma hata katika maandalizi yao.

Akifafanua kuhusu mkutano kati ya Baba Mtakatifu na Viongozi kutoka Milano, Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema kwamba, Baba Mtakatifu ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na jinsi ambavyo onesho la kimataifa huko Milano, litaweza kutoa fursa za ajira kwa vijana ambao kwa sasa wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira, jambo ambalo linaonekana kwa sasa kuwa kama ni janga la kitaifa na kimataifa!







All the contents on this site are copyrighted ©.