2014-01-18 09:30:05

Askofu mkuu Ruwa'ichi awataka watanzania kuacha tabia ya ukatili, unafiki na kuwachafulia wengine majina yao!


Kizazi cha Nyakati za sasa kiache unafiki na ukatili kwa kujiona kuwa ni bora zaidi kila mmoja kwa kumsontea kidole mwingine, kwa kutangaza udhaifu wa wengine na kudhalilishana. Ameyasema hayo Askofu Mkuu Yuda Thaddei Ruwa’ichi, wa Jimbo Kuu la Mwanza, katika Misa Takatifu ya kumsindikiza katika safari ya mwisho Pd. Pius Bilulu tarehe 16 Januari 2014, katika Kanisa Kuu la Epifania, Bugando Jimbo kuu la Mwanza.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wanadamu leo wamekosa huruma na kupendelea kuangamiza wengine kwa kuwachafulia sifa zao, au kuwadharirisha kwa kutangaza udhaifu wao hadharani na kushinikiza wawajibishwe vibaya kutokana na yale wanayowatuhumu. Tabia hizi husababishwa na hisia za watu hawa kudhani kuwa wao ni wenye haki sana, ni waadilifu sana, hawana dhambi. Kwa ufupi watu wa namna hii hujiona kuwa ni wakamilifu na wenye mastahili zaidi kuliko wengine. Huu ni unafiki mkubwa wanaopaswa kujiepusha nao, amewaasa Askofu Ruwa’ichi.

Badala ya kunyosheana vidole na kutafuta kudhalilishana, yafaa kila mmoja ajitambue kuwa ni dhaifu na ajiaminishe kwa Mwenyezi Mungu, aliye Mungu wa Huruma, Upendo na Haki. Wale wanaotafuta kuanika udhaifu wa wengine, hawapishani na mafarisayo wanaomshutumu kwa Kristu, mwanamke mdhambi ili auwawe kwa kupondwa mawe. Kristo mwenye Huruma, Upendo na Haki anawakumbusha: “Asiye na dhambi ndiye awe wa kwanza kurusha jiwe” (Rej. Yohane 8,7). Kwa hakika hakuna mwenye kujihesabia haki ya kuhukumu wengine. Ndiyo sababu simulizi laeleza kuwa baada ya Kristu kuinua macho alikuwa kabaki yule mwanamke peke yake na washitaki wake wote wameondoka kwa kutambua kuwa wao pia ni wadhambi. Kwa Upendo, Huruma na Haki, Kristo anamwambia: “wala mimi sikuhukumu, nenda zako, wala usitende dhambi tena” (Rej. Yohane 8,11).
Zinahitajika jitihada za kutokutenda dhambi kwa kuepuka nafasi zinazompelekea mwanadamu kuanguka dhambini na kisha kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Aidha kila mmoja ajifunze kwa tendo la Kristo anapowaosha miguu wanafunzi wake (Rejea Yohane 13, 5). Tendo hili lifungue macho ya wanadamu wote kuhangaikia usafi wa wengine, kuhangaikia utakatifu na wokovu wa wengine na sio kuhangaikia maangamizi yao.
Kwa hakika Padri Pius Bilulu hakuwa mkamilifu, lakini pia hakuwa shetani, bali alikuwa mfuasi wa Kristu, mwenye hadhi ya binadamu, hali ya udhaifu, haki ya kuwa mwana wa Mungu, na haki ya ukombozi. Mwanadamu anayepambana na madhaifu yake na jitihada za kuongoka. Hizi ndizo sifa za utakatifu: kwamba ingawa mwanadamu yu na hali ya udhaifu, mwanadamu ajitambue na kuhangaikia kuongoka kwake akijiaminisha kwa Mungu. Amesisitiza Askofu Ruwa’ichi.
Padri Pius Bilulu katika maisha na utume wake alionesha kila ishara za kujiaminisha kwa Mungu na kuahangaikia wokovu wake na wa wengine. Askofu Ruwa’ichi amewaalika waamini na wote wenye mapenzi mema kuungana na kilio cha Mzaburi wakiwa wanamwombea Padre Bilulu kwa imani kuwa ni kilio chake pia: “Toka upeo wa unyonge wangu nakulilia ee Mwenyezi Mungu. Ee Bwana sikia sauti yangu, uitegee sikio sauti ya ombi langu. Kama ee Mwenyezi Mungu ungehesabu makosa yetu, nani ee Bwana angeweza kusalimika? Lakini kwako tunapata msamaha, ili sisi tukuheshimu” (Rej. Zaburi 130, 1-4).
Padri Pius Bilulu alizaliwa tarehe 30/01/1943 katika kijiji cha Itira, wilayani Ukerewe, Mwanza. Akapewa daraja la Upadri 1971 na Askofu Renatus Butibubage. Alifanya utume wake katika parokia na taasisi mbalimbali za Jimbo Kuu la Mwanza mpaka 2013 alipopumzika kufuatia hali yake ya afya. Ameanza kuugua tangu 2005 na amefariki tarehe 13/01/2014 kwa ugonjwa wa kifua kikuu, alipokuwa amelazwa Hospitali ya rufaa ya Bugando.
Raha ya Milele uumpe ee Bwana, Apumzike kwa amani.. Amina.

Habari hii imeandaliwa na Pd. Celestin Nyanda.
Jimbo kuu la Mwanza. Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.