Papa awapongeza wafanyakazi wa Vatican kwa moyo wa kujisadaka, weledi na bidii ya
kazi!
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014 ameendelea kukutana na kuzungumza
na wafanyakazi wanaotoa huduma ya kutayarisha na kupamba maua sehemu mbali mbali za
mji wa Vatican na katika matukio ya maisha na utume wa Kanisa mjini Vatican. Hawa
ni wafanyakazi wanaofanya ukarabati katika majengo ya Vatican, jambo linalohitaji
moyo wa kujisadaka na uvumilivu mkuu.
Baba Mtakatifu anawapongeza kwa moyo
na bidii ya kazi hasa katika kupanga viti wakati wa Ibada kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro na wakati wa Katekesi zake, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican. Hii ni kazi inayotekelezwa kwa tija, weledi na majitoleo makubwa.
Baba
Mtakatifu Francisko anawahimiza wafanyakazi wa mapambo na ukarabati kuendelea kutekeleza
utume wao katika hali ya utulivu, matumaini na kusaidiana. Mwelekeo huu wa utendaji,
utakuwa na tija kubwa kwa Jumuiya nzima ya wafanyakazi wa Vatican. Baba Mtakatifu
amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka wafanyakazi pamoja na familia zao chini ya ulinzi
na usimamizi wa Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi.