Watanzania wanaomboleza kifo cha Jaji George Liundi, Msajili wa kwanza wa Vyama vya
Siasa Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesikitishwa na kuhuzunishwa
na kifo cha ghafla cha aliyekuwa msajili wa kwanza wa vyama vya siasa nchini, Jaji
George Liundi kilichototokea Januari 12, 2014, nyumbani kwake Keko, mjini Dar Es Salaam.
Katika
salamu zake za rambirambi ambazo alizituma kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji
Francis Mutungi, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea taarifa cha kifo cha Bwana Liundi
kwa masikitiko na huzuni. “Bwana Liundi alikuwa mtumishi mtiifu wa umma, alikuwa mchapakazi
wa kuaminika na alikuwa mwandishi hodari wa sheria. Tutamkumbuka kama mtumishi mwadilifu
na mwaminifu wa umma na mfano wa kuigwa wa utumishi bora,” amesema Rais Kikwete katika
salamu zake za rambirambi na kuongeza:
“Nakutumia wewe Msajili wa Vyama vya
Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi salamu zangu za rambirambi, nikiungana nawe kuomboleza
kifo cha Bwana Liundi. Aidha, kupitia kwako nawatumia wanataaluma wote wa sheria nchini
salamu nyingi za rambirambi kwa kuondokewa na mwenzao.”
Ameongeza: “Napenda
vile vile kupitia kwako unifikishie pole nyingi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia wa
Marehemu Liundi ukiwajulisha kuwa niko nao katika masikitiko na majonzi ya msiba huu
mkubwa. Wajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na namwomba Mwenyezi
Mungu awape nguvu na subira kuweza kuvuka kipindi hiki kigumu. Aidha, naungana nao
katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze peponi roho ya Marehemu
George Liundi. Amen.”