2014-01-16 09:34:42

Taharuki ya Mtakatifu Yosefu! Mtu wa haki!


“Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa hivi. Maria mama yake, alipokuwa mchumba wa Yosefu, kabla hawajakaa pamoja alionekana na mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mumewe Yosefu akiwa mtu mwadilifu, hakupenda kumwaibisha hadharani. Basi akanuia kumwacha kwa siri.”
(Mt 1:18-19)

Moja ya kifungu cha maneno chenye utata mwingi kwa wasomaji wa Injili ya Matayo ni 1:18-19. Haya mbili lakini zina mambo mengi. Mfano mdogo tu ni kuwa uhusiano wa Maria na Yosefu, unaelezewa kwa maneno matatu yenye utata. Kwanza walikuwa wamechumbiana, pili, Yosefu amenuia ‘kumwacha kwa siri’ yaani kumpa talaka na tatu, tunaambiwa Yosefu ni mume wa Maria. Kueleya haya tunapaswa kuingia katika ulimwengu wa utamaduni wa Kiyahudi, mintarafu mambo ya ndoa.

Katika mila na desturi za Wayahudi mintarafu ndoa, ilikuwa na sehemu mbili. Kwanza ni tendo la mume kwenda kumposa mwanamke. Hatua hii ilichukuliwa katika upekee wake na ilikuwa na matokeo ya kisheria (soma Kumb 20:7; 22:23-27). Tukio hili lilipangwa na wazee wa koo husika. wanandoa hawa kwa kawaida walikuwa katika umri mdogo, kwa kipindi cha Yosefu na Maria, mwanaume alikuwa na miaka kumi na tatu na mwanamke kumi na mbili.

Ukiachia na mahusiano ambayo yaliharamishwa kati ya ndugu (soma Law 18), ilikuwa ni kawaida kwa kuoana ndani ya kabila na hata familia. Shughuli ya uposaji ilifanyika nyumbani kwa baba wa bibiarusi, na ndipo alipaswa kuendelea kuishi. Bwana arusi alitoa mahari. Miaka kadhaa ilipita kabla hatua ya pili, ambayo ni ya mwisho kufikiwa.

Hatua ya pili, ndoa yenyewe. Tukio hili lilihusisha kuchukuliwa kwa mke toka nyumba ya wazazi wake kwenda kwenye nyumba ya mume wake au ya baba mkwe. Tunaposoma Mt 1:18-25, ni wazi kwamba hatua ya kwanza ilishafanyika katika ya Yosefu na Maria, walikuwa wanasubiri tu sherehe ya ndoa yenyewe. Maria alikuwa amebaki nyumbani kwa wazazi wake, na Yosefu alikuwa na haki ya kumtembelea kila alipopata nafasi. Kabla ya kufunga ndoa, yaani mke kwenda rasmini nyumbani kwa mume, kulikuwa na kipindi cha miezi isiyozidi kumi na mbili ya uchumba. Katika kipindi hiki cha mpito cha uchumba, wahusika walikuwa wanachukuliwa kama mke na mume.

Swali wanaojiuliza wanataaluma wa Maandiko Matakatifu, ni je, Yosefu alisafiri pamoja na Maria alipokwenda kumtembelea Elizabethi? Swali hili linajitokeza kwa kuwa katika simulizi la safari ya Maria kwenda Hebroni kumtembelea na kumsaidia shangazi yake Elizabethi ambaye katika uzee wake alikuwa mjamzito, jina la Yosefu alitajwi.

Hebroni ulikuwa mmoja wa miji ya kikuhani na mji wa ukimbizi. Ndio mji ambao Abrahamu alipoingia nchi ya Kaanani aliweka hema lake (Mwz 13:18). Mahali alipowapokea Malaika watatu wageni, waliompatia ahadi kwamba kwa mzao wake mataifa yote ya duniani yatajibariki. Mji huu ndio ulikuwa na mifupa ya Abrahamu, Isaka, Yakobo, Sara, Rabeka na Lia ambayo ilizikwa katika pango la Efroni (Mwz 25:9, 10; 49:29-31), kwa hakika Yosefu na Maria walipokuwa wakipita katika mji huu, wahenga hawa wafarijika.

Ni kwa hakika kwamba Mwinjili hasemi kwamba Yosefu alikuwa pamoja na Maria katika safari hii. Ila pia hasemi kwamba hakuwepo, wala kwamba Maria alienda Hebroni pekee yake. tunachojua kwamba safari ya kwenda kwenye nchi hii ya milimani, haikuwa safari nyepesi, na tena Maria alikuwa wa umri mdogo. Hivyo kuifanya safari hii peke yake, lilikuwa ni jambo la hatari sana.

Kwa hakika jukumu la Yosefu katika maisha ya Maria ni kuwa mlinzi, kiongozi na mlezi. Jukumu hili, Yosefu alilichukua kama wajibu wake mkuu. Ni jambo lililoweza kufikiriwa kwamba katika nafasi ya kwanza muhimu ambayo jukumu la Yosefu lilipaswa kuonekana, yeye aliingia mitini! Hivyo kwa hakika Yosefu alikuwa mwenza wa Maria katika safari yake ya kwenda Hebroni, kuwatembelea Elizabethi na Zakaria, kuwasaidia na kuwatia moyo. Walikaa na kuwasaidia wazee hawa mpaka Elizabethi alipojifungua na siku nane baadaye mtoto wao kutahiriwa, ndio walipoanza safari ya kurudi kwao.

Yosefu na Maria baada ya kurudi Hebroni, siku moja ukweli kwamba mke wake maasumu sana alikuwa mjamzito uligusa akili yake. Yosefu alikuwa na yakini kwamba Maria ni mjamzito. Mwinjili Mathayo anatuambia hivi Maria: “alipokuwa mchumba wa Yosefu, kabla hawajakaa pamoja alionekana na mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.”

Mt. Yeronimo anajiuliza mwenyewe “Ni nani aliyegundua?” Ni dhahiri hapa muhusika ni Yosefu, ndiye aliyegundua. Watu wengine kamwe wasingeweza kufikiria kuwa amepata mimba kwa uwezo wa kiungu, wao walijua tu kuwa ni matokeao ya kawaida ya ndoa halali, lakini fikira haikuwa hivyo kwa mumewe. Yosefu alijua kwa hakika kuwa Maria alikuwa na ubikira usio na mawaa. Zaidi ya hili, alifahamu kwa kina sana utakatifu wake usioingilika. Yosefu alijua kwamba Maria anaishi maisha ya kimalaika hapa duniani.

Kwake lilikuwa wazo la ajabu, je Maria ndiye mama wa Masiya, bikira aliyetabiriwa na nabii Isaya? Bikira ambaye atamzaa Imanueli? Twapaswa kujua kwamba Yosefu aliyafahamu kwa kina Maandiko Matakatifu. Mt. Fransisko wa Sale anamwagia sifa Mt. Yosefu kuwa alikuwa na hekima zaidi ya Selemani.

Si tu Mt. Yosefu lakini Wayahudi wengi wa wakati wake walikuwa wakisubiri kwa hamu ujio wa Mwokozi, Mt. Luka anatutajia wawili Mzee Simoni na nabii wa kike Ana, binti Fanueli (2:25, 36). Hawa wote waliokuwa wakimsubiri walijua kuwa atakuwa wa kabila Yuda na wa nyumba ya Daudi. Wale wote walioujua unabii wa Isaya, walijua kuwa atazaliwa na bikira.

Je mambo haya yote kwa pamoja si yalimfanya Yosefu awe ana ushahidi tosha kuhusiana na fumbo lililoendana na hali aliyokuwa nayo Maria? Wazo hili lililoingia akilini mwake, ambalo kwa wengi lingeweza kuhamsha hisia za kujiona, kuzua kiburi na kumfanya awe na majivuno, lakini kwa mnyenyekevu wetu huyu, ukweli huu ulimsababishia taharuki nafsini mwake.

Twaweza kabisa kuvuta fikra zetu na kumwona katika kibanda chake cha uselemara, randa yake ameiweka pembeni, akijiuliza: “Mama wa Mungu ndiye mke wangu? Mwana wa Baba wa mbinguni azaliwe katika nyumba yangu!” Kwa haki dhamiri yake ilimwambia heshima hiyo hakuistahili. Mwana wa Mungu, nafasi yake si katika nyumba yake!

Je, aendelee kumkubali, kumtambua na kumchukulia Maria kama mke wake, huyu aliyechukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu? Je aje kumdai ni mtoto wake Yeye aliye mtaktifu ambaye atazaliwa na Maria? Alisinyaa kutokana na fadhaa takatifu kutokana na wazo hili.

Kwa hakika Maria na Yesu, sehemu yao haikuwa katika nyumba yake! shida afanye nini katika hali hii? Je kimya kimya aondoke na kwenda kujificha jangwani na katika unyamavu wa Jordani, nafsi yake ikalie kuwa kutostahili kwake kukaa na makuu haya! Hii ndio ulikuwa taharuki ya Yosefu alipotambua Maria ni mjamzito na wala sio shaka na wasiwasi wenye kuhuzunisha juu ya uaminifu wa mke wake maasumu.

Tuone kwa kina ushahidi wa jambo hili. Mwinjili Matayo anatuambia dhahiri kuwa Maria alionekana na mimba ya Roho Mtakatifu (1:18, 19). Maelezo haya Yosefu peke yake ndiye ambaye angeweza kuyatoa, kwani ndiye aliyekuwa na uhakika kwamba wao hajakaribiana, mimba ya Roho Mtakatifu, kwa hakika hapa tunaambiwa wawili hawa walikubaliana juu ya maisha ya usafi wa moyo. Jambo moja hapa lipo wazi, Yosefu inasisitizwa kuwa ni mume.

Hivyo hatua ambayo walikuwa nayo Yosefu na Maria ni ya ndoa, japokuwa walikuwa hawajakamilisha hatua ya mwisho ya mume kumchukua mke nyumbani kwake.

Kama ndoa yao ingekuwa umefungwa mara baada ya kutokewa na Malaika, jambo hili lisingekuwa la heshima kwa Maria, kwani Yesu angezaliwa miezi sita baada ya ndoa, kioja ambacho kisingesahaulika na wana Nazarethi. Lakini tuna uhakika na uhalali wa kuzaliwa kwa Yesu hakuna aliyeutilia shaka, hata maadui zake, ambao wangeweza kuutumia uvumi, kama ungekuwepo.

Mwinjili anaendelea kutuambia Mumewe Yosefu akiwa mtu mwadilifu, hakupenda kumwaibisha hadharani. Basi akanuia kumwacha kwa siri, kumwacha Maria, kwa maneno mengine ‘kujitenga naye’ kwani neno linalotumika katika Vulgate ni dimittere, lina maana hii pia. Katika Mt. 19:5, “Kwa hiyo mtu atamwacha baba na mama...” neno dimittet alimaanishi talaka au kutelekeza. Yosefu asingeweza kumwacha Maria kwa talaka ya siri, au kwa njia nyingine yoyote, bila jambo hili kujulikana na hivyo kuchafua jina la Maria, jambo ambalo Yosefi hakupenda litokee.

Hapa tunapaswa kumwangalia upya Yosefu ambaye ni mtu “mwadilifu” yaani mwenyehaki, jambo ambalo tunaambiwa ndio msingi ambao ulimfanya atende alichotaka kukitenda. Aya hii haituambii kuwa Yosefu alikuwa mwenyehuruma, hatuambiwi kuwa alikuwa mpole, wala haitupatii neno lenye kuonesha kwamba alikuwa tayari kusamehe au kupuuzia kwa upande wake. Tunaambiwa tu kwamba alikuwa mwenyehaki.

Neno haki, Mt. Yeronimo anatoa maana yake kuwa ni kuwa na ukamilifu wa fadhila zote. Inaonesha kutekeleza kiaminifu maagizo yote ya Sheria ya Mungu. Mwinjili Luka anawaelezea Zakaria na Elizabethi “Wote wawili walikuwa wachamungu, katika maisha yao amri zote za Bwana na sheria zake zote” (1:6), yaani watekelezaji wa Sheria zote za Musa. Lakini Sheria ya Musa haikumwachilia huru kubaki na mke wake aliye na hatia ya uzinzi au hata kuficha uhalifu wake, kama umejulikana kwake.

Kama Yosefu hakumwacha Maria, na alitamani asielekezewe wasiwasi wowote, inamaanisha hakuwa na shaka kwamba hakuwa mwaminifu ama sivyo sifa ‘mwenyehaki’ isingeweza kutumika kwake, kwani hasingeweza kuwa mtimiza Sheria kwa kujua dhambi ya mwenzake na kuficha (soma Law 5:1; Mith 18:22). Hivyo kama kwa kuwa na ufahamu wa dhambi na kuficha, mtu aliwekwa chini ya adhabu ya dhambi, Yosefu asingeweza kuitwa mwenyehaki.

Kutokana na uenyehaki wake, Yosefu hakuwa tayari kumwacha Maria, kwani alijua juu ya kutokuwa kwake na hatia. Na kama ana mtoto, itakuwa ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Lakini kama Maria hana hatia kwa nini abaki naye?

Yosefu alishawishika kwamba kutokana na ishara zote alizoziona, kwamba Maria ni mama wa Masiya, na aliona kuwa yeyeyhastahili kukaa chini ya dri moya na mama huyu na pia na Tamaa ya Mataifa yote, ndio maana aliamu aondoke kwa siri, ili kwamba sifa yake isiharibiwe. Angemwacha hadharani, maswali mengi yanguibuka juu ya tendo hili. Lakini kuondoka kimya kimya watu wangewaza tu kuwa kutokana na kazi yake, amepata kazi mbali na kwao. Hii ilikuwa kwake safari mpya ya kwenda Yudea.

Bado twaweza kujiuliza wenyewe, Yosefu angepata wapi moyo wa kumwacha mke wake mpendwa sana, na aliyekuwa katika hali ya ujauzito? Kumtelekeza bila ya mtu wa kumsaidi na bila msaada wowote katika shida yake? Je alifikiria huzuni ambayo Maria angekuwa nayo? Kwa hakika Yosefu aliyawaza haya yote. Lakini kicho na uchaji ambao alikuwa nao mbele uwepo wa Mungu Mwilika vilikuwa na nguvu ndani yake kuliko upendo na wema aliokuwa nao kwa mkewe. Bila kukoma kumpenda mkewe, alitafakari na kuona kwamba kujificha mbali ndio jibu la taharuki yake, kwani Maria kuwa na Mungu alishakuwa na msaada wa kutosha, usalama, faraja na mwenza bora zaidi, kuliko vile yeye alivyoweza kumpatia. Utengano huu ulikuwa sadaka kwake, na ulimsababishia maumivu ambayo hayasemeki, lakini kwake yalikuwa ya muhimu, ndio maana alinuia kujitenga.

Waalimu mashuhuri wa Kanisa wanakubaliana na ufafanuzi huu wetu (Aimoni, Mt. Toma, Isidoro Isolano, Orijeni, Yeronimo, Basili Remigio, Theophilact, Mt. Bernard na Gerson). Mt. Bernardi anajiuliza: Sababu gani ilimfanya Yosefu afikirie kujitenga na Maria? Sababu iliyomsukuma Yosefu kutaka kujitenga na mkewe ni sawa na Petro alivyotaka ajitenge na Bwana: “Ondoka kwangu, ewe Bwana, kwa maana mimi ni mtu mkosefu” (Lk 5:8).

Ni sawa na Jemedari alivyomtaka Yesu asiingie katika nyumba yake “... Bwana, usijisumbue, maana sistahili uingie chini ya dari yangu...” (Lk 7:6). Vivyo hivyo Yosefu alijiona kuwa yeye aliye mdhambi hastahili kuishi na mtukuka huyu, mwenye heshima ya hali ya juu kabisa, jambo ambalo lilileta kicho ndani yake. yosefu hakuweza kulielewa fumbo ambalo Maria alikuwa analibeba, ndio maana alitamani kumwacha.



Je, tunashangaa tunapomwona Yosefu akishangaa alipotazama ujauzito wa mke wake, na kuwa na uhakika kwamba hastahili kukaa na bikira maasumu huyu? Tumsikilize japo kidogo Mt. Elizabethi, ambaye hakuweza kustahimili uwepo wa Maria, bila tetemeko na uchaji mkuu na alipaza sauti yake “Kutoka wapi imenifikia heshima ya kutembelewa na mama wa Bwana wangu?” (Lk 1:43).

Maelezo ya Mt. Bernard hayahitaji kufafanuliwa zaidi. Remigio anasema Yosefu anaona kwamba mkewe ni mjamzito, ana mwona Mtoto, yeye anayemjua kuwa ni bikira; na kwa sababu alisoma kutoka kwa nabii “Chipuko litatoka katika shina la Yese, kitawi kitaota katika mizizi yake” (Isa 11:1). Hakuuliza wala kuwa na shaka juu ya ubashiri huu kuwa wakaribia kutokea katika Maria. Anaendelea kueleza: Inawezekana zaidi kuwa Yosefu aliamini kwamba mwanamke anaweza kushika mimba bila mchango wa mwanaume, kuliko kwamba Maria anaweza kutenda dhambi.

Mt. Toma anasema “Mt. Yosefu alifikiri katika unyenyekevu wake asiendelee kuishi na utakatifu huu mkuu.” Mt. Fransis wa Sale naye anatuambia akiakisi maneno ya Mt. Bernado unyenyekevu wa Mt. Yosefu, kama anavyofafanua Mt. Bernado, ulikuwa ni sababu ya kutamani kumwacha mama yetu alipofahamu kwamba ana mtoto . Mt. Bernardo anasema kwamba alifikiri hivi nafsini mwake: “Hili ni nini? Nafahamu kwamba ni bikira kwani pamoja naye tumejiwekea ahadi ya kutunza ubikira wetu na usafi wetu wa moyo, jambo ambalo kwa hakika hajalishindwa.

Lakini kwa upande mwingine, naona kwamba ana mtoto. Na inawezekanaje umama na ubikira vikakaa pamoja? Kwa nini ubikira usiwe kikwazo kwa umama? Je, yawezekana, kuwa yeye ndiye bikira mtukufu ambaye nabii amemtangaza kwamba atapata mimba na kumzaa Masiya? Kama ni hivi, ni vyema mimi kutoishi pamoja naye, mimi nisiyestahili kufanya hivyo. Ni vyema kwa kificho nimwache kutokana na kutostahili kwangu na nisiishi tena katika umoja naye. Haya ni mawazo ya ajabu ya mnyenyekevu wetu huyu wa mfano.

Taharuki hii ya Mt. Yosefu, inatufunza jambo moja kuu katika maisha, kuwa waaminifu katika miito yetu. Maisha yetu yanapaswa kuwa safi, kwamba hakuna mtu anayeweza kututilia shaka ya jambo lolote lililo baya. Mwenendo wetu mbele ya Mungu na mbele ya jamii, iwe palipo na mwanga au palipo na giza, uwe usio na mawaa!

Kwa hakika Bwana ujibu sala za wacha Mungu wake, na ndiyo ilivyotokea kwa Yosefu. Kwani katika taharuki hii yote, bado aliyaweka matumaini yake kwa Mungu. Alijifungua moyo wake mbele yake. Taharuki yake aliizamisha katika tafakari ya kina. Ndio maana Malaika wa Bwana akamtokea kwa ghafla na kumweleza yaliyokuwa maagizo ya Mungu kwake: “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumpokea Maria kuwa mke wako, maana mimba yake ameipata kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Tafakari hii imetayarishwa na
Padre Stefano Kaombe,
Jimbo kuu la Dar es Salaam.







All the contents on this site are copyrighted ©.