Nyumba ya Papa ni mali ya Wakatoliki wote, mahali pa kuonja upendo, ukarimu na kuimarisha
imani!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 16 Januari 2014 amekutana na kuzungumza
na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na utume wao kwenye Makazi ya Papa mjini Vatican.
Baba Mtakatifu amewashukuru kwa huduma na ukarimu wanaowashirikisha wageni mbali mbali
wanaofika mjini Vatican kwa ajili ya kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Nyumba ya Papa ni mali ya Waamini wote
wa Kanisa Katoliki; mahali ambapo wanaonja tone la upendo na moyo wa ukarimu wa kifamilia
pamoja na msaada wa kulinda na kudumisha imani ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu. Mmiliki mkuu wa Nyumba ya Kipapa ni Yesu mwenyewe na wengine wote ni wafuasi
na wahudumu wa Injili.
Baba Mtakatifu anasema kutokana uelewa huu, kuna haja
kwa wafanyakazi hao kukuza na kudumisha majadiliano ya kina kwa njia ya sala, ili
kuimarisha urafiki na uhusiano wa ndani kabisa, tayari kutolea ushuhuda wa upendo
na huruma ya Mungu kwa watu wake. Wafanyakazi hawa anasema Baba Mtakatifu wanapotekeleza
utume wao, kazi inaweza kuwa ni fursa ya kuwashirikisha wengine furaha ya kuwa ni
sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Baba Mtakatifu anawaalika
kuwa makini katika kuisikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu inayowaita kila siku, kumtumikia
kwa ukomavu na moyo wa ukarimu. Baba Mtakatifu amewatakia wafanyakazi hawa pamoja
na familia zao, kheri na baraka kwa Mwaka Mpya 2014.