2014-01-16 07:53:14

Majadiliano ya kina na vyama vya upinzani yalenge kwenye upatanisho wa kitaifa na mafao ya wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linaishauri Serikali kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kina na vyama vya upinzani ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, haki na amani pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. RealAudioMP3

Kuna haja kwa Serikali kushirikiana na wadau mbali mbali katika kutoa elimu na majiundo makini kwa vijana, ili waweze kutambua tunu msingi za maisha ya ujana, tayari kuzitumia kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa na taifa kwa ujumla.

Vijana kwa sasa wanakabiliwa na tatizo la matumizi haramu ya dawa za kulevya, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na mmong’onyoko mkubwa wa maadili na utu wema, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa taifa. Maaskofu wanasema, kuna haja kwa Serikali kukutana na kujadiliana na vyama vya upinzani, vyama vya wafanyakazi na wadau wengine ili kujadili mustakabali na hatima ya taifa la Venezuela, tayari kuanza ukurasa mpya wa ushirikiano, kuliko hali ilivyo kwa sasa kwani wanasiasa wa upinzani wanaiangalia Serikali kwa jicho la makengeza!

Maaskofu Katoliki Venezuela katika Waraka wao kwa Serikali, wanaonesha wasi wasi kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya jinai, ukosefu wa amani na usalama; kuporomoka kwa ubora wa huduma ya afya na elimu nchini humo; ukosefu wa dawa muhimu na kwamba, wananchi wengi wanaendelea kutumbukia katika hali ya umaskini wa kutupwa kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma inayotolewa nchini Venezuela. Bei ya mazao ya chakula imeongezeka maradufu kutokana na uchu mali na utajiri wa haraka haraka unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara nchini humo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linapinga mkakati wa Serikali wa kutaka kuwapokonya wananchi uhuru wa kujieleza na kupata habari, kinyume cha Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama. Maaskofu pia wanapinga sera za serikali kutaka kubadilisha mitaala ya masomo kwa kujikita zaidi katika masuala ya kisiasa badala ya kutoa fursa kwa wanafunzi kujipatia ujuzi na maarifa ili kuweza kupambana na hali mbali mbali za maisha huko duniani. Sera ya elimu inataka kuwanyima wazazi uhuru wa kuchagua elimu na malezi kwa watoto wao.

Maaskofu wanasema, kuna haja ya kuendelea kutoa elimu ya dini shuleni ili kuwafunda watoto katika maadili na utu wema, tayari kushiriki katika mchakato wa kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi yao, huku wakiwa ni wachamungu.

Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali kwa miaka ya hivi karibuni umeendelea kusuasua, kutokana na Kanisa kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: haki msingi za binadamu, amani na mafao ya wengi mambo ambayo yamekuwa yakiichefua Serikali ya Venezuela.








All the contents on this site are copyrighted ©.