Khalifa wa Mtakatifu Petro si kikwazo cha majadiliano ya kiekumene bali ni daraja
linalounganisha juhudi za kiekumene!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuimarisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa
Wakristo na kwamba, hivi ni kati ya vipaumbele vyake katika maisha na utume wa Kanisa
katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Hivi ndivyo anavyobainisha
Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo, wakati
huu Wakristo wanapojiandaa kuanza Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2014,
unaongozwa na kauli mbiu " Je, Kristo amegawanyika? Sehemu ya Waraka wa kwanza wa
Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho 1: 1-17. Itakumbukwa kwamba, Juma la kuombea Umoja
wa Wakristo lianza tarehe 18 hadi tarehe 25 Januari, Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtume
Paulo mwalimu wa Mataifa.
Kardinali Koch anasema, tema hii inakwenda sanjari
na hija ya sala ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24
hadi tarehe 26 Mei 2014, kama kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Miaka 50 tangu Papa Paulo
VI alipotembelea Nchi Takatifu. Akiwa huko, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana
na kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox.
Juhudi
zinaendelea kufanyika ili kuangalia uwezekano wa Baba Mtakatifu Francisko kukutana
na kuzungumza na Patriaki Kiril wa Moscow, Russia. Kama wazo hili litaweza kuzaa matunda
yanayokusudiwa, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Papa kukutana na kuzungumza na Patriaki
wa Kanisa la Kiorthodox la Russia.
Kardinali Kurt Koch anasema, tangu baada
ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Viongozi wakuu wa Kanisa wameendelea
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa umoja na mshikamano wa Kanisa kwa kukazia majadiliano
ya kiekuemene, ili Wakristo wawe wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu. Kumbe, kuhusu
dhamana na nafasi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mchakato wa majadiliano ya
kiekumene si kikwazo bali ni daraja linalounganisha juhudi za Kiekumene.