2014-01-15 08:29:51

Ujumbe wa Vatican na Marekani wakutana ili kujadili kuhusu mchakato wa amani nchini Syria


Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 14 Januari 2014 mjini Vatican, amekutana na kufanya mazungumzo na Bwana John Kerry, Katibu wa Nchi wa Marekani ambaye ambaye anaendelea kuhamasisha kuhusu Awamu ya Pili ya Mkutano wa Amani nchini Syria, unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 22 Januari 2014.

Akizungumzia kuhusu mkutano huu, Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, umewahusisha pia viongozi waandamizi kutoka Ubalozi wa Marekani mjini Roma na kutoka katika Mabaraza ya Kipapa yanayojihusisha na tema iliyokuwa inajadiliwa. Viongozi hawa wamejadili kwa kina na mapana hali halisi ilivyo kwa sasa huko Mashariki, lakini kwa kuweka mkazo zaidi huko Syria, ambako watu wanaendelea kukabiliana na maafa ya kutokana na vita.

Vatican imeonesha wasi wasi na matumaini kwa ajili ya kupata suluhu ya amani nchini Syria, kama ilivyofafanuliwa pia na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican mapema siku ya Jumatatu. Wamekubaliana kimsingi kwamba, kuna haja bado ya kuendelea kutoa misaada ya kiutu kwa wananchi wa Syria. Wamegusia pia majadiliano kati ya Israeli na Palestina ili muafaka uweze kufikiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa pande hizi mbili.

Vatican imemwelezea Bwana John Kerry wasi wasi wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Marekani kuhusiana na sera ya mageuzi katika sekta ya afya na umuhimu wa kulinda na kutetea uhuru wa kidini na dhamiri nyofu. Wamezungumzia pia mikakati ya Rais Barack Obama wa Marekani katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato nchini Marekani, hususan miongoni mwa wananchi wenye kipato cha chini.

Padre Federico Lombardi anasema kwamba, hali ya mkutano kwa ujumla ilikuwa ni ya kirafiki na kwamba, mkutano huu umekuwa na manufaa makubwa kwa ajili ya kudumisha na kukuza ushirikiano wa kimataifa, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kimsingi, wajumbe wamejadili mambo muhimu yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa wakati huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.