2014-01-15 14:42:04

Jumuiya ya Kikristo ni muhimu sana katika maisha, ushuhuda na Uinjilishaji: Wakristo wanakuwa ni Wafuasi na Wamissionari


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 15 Januari 2014 ameendelea kutoa Katekesi Mpya kuhusu Sakramenti za Kanisa. Akizungumzia kuhusu Sakramenti ya Ubatizo, Baba Mtakatifu anasema kwamba, ni Sakramenti inayomwezesha mwamini kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa pamoja na kushiriki dhamana ya kuwa ni sehemu ya Wana wa Mungu; watu wanaofanya hija katika historia ya maisha ya mwanadamu.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanarithishwa maisha ya uzima wa milele kwa njia ya Maji ya Ubatizo na Roho Mtakatifu na hivyo kujaliwa neema ya kutembea katika nyakati kama mto unavyomwagilia maji ardhi na kueneza baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanawezeshwa kuwa ni Wamissionari, wanaoitwa kutangaza Injili ya Kristo duniani kote. Kila Mkristo ndani ya Kanisa ni mdau wa Uinjilishaji Mpya, changamoto kwa kila mwamini. Familia ya Watu wa Mungu anasema Baba Mtakatifu ni Wafuasi na Wamissionari kwa daima kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake ndani ya Kanisa kadiri alivyokabidhiwa na Kristo mwenyewe.

Wakristo wanapopokea Ubatizo wanakirimiwa pia wito wa kimissionari na ushiriki wa Kimungu kwa njia ya Roho Mtakatifu anayewapatia ujasiri wa kumkiri Yesu Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu pamoja na kumwita Mwenyezi Mungu, Abba, yaani Baba, mwaliko wa kuishi na kuwashirikisha wengine umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Kama Jumuiya ya Waamini wanaonja mang'amuzi ya upendo na wanachangamotishwa kuwa ni vyombo vya neema kwa jirani zao, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu na uwepo wa dhambi. Dhana ya Jumuiya ya Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Maisha ya Kikristo, Ushuhuda na Uinjilishaji. Imani ya Kikristo inapata chimbuko lake ndani ya Kanisa na inaendelea kumwilishwa ndani ya Kanisa. Katika Sakramenti ya Ubatizo waamini wanasherehekea kuzaliwa kwa mwanajumuiya mpya ndani ya Kristo na hivyo kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wake, Yaani Kanisa.

Baba Mtakatifu katika Katekesi yake kuhusu Sakramenti za Kanisa anasema kwamba, Jumuiya ya Kikristo nchini Japan ni mfano wa kuigwa. Ilikumbana na madhulumu mwanzo mwa Karne ya kumi na saba. Hapa waamini wengi wakayamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Makleri wakafukuzwa kutoka Japan na watu wengi wakapoteza maisha yao. Lakini Wakristo wakaenda mafichoni, wakaendelea kuhifadhi imani yao katika sakafu za mioyo yao, wakairutubisha kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu.

Baada ya Karne mbili hivi, Wamissionari wakabahatika kurejea tena nchini Japan; wakristo wakajitokeza hadharani wakiwa na ari na nguvu mpya. Wakristo waliweza kuendelea kuishi kutokana na neema ya Ubatizo. Walijenga na kudumisha moyo wa Kijumuiya, kwani Sakramenti ya Ubatizo ilikuwa imewaunganisha pamoja na hivyo kuwa ni mwili mmoja wa Kristo: Walitengwa na kujificha, lakini walibaki daima kuwa ni viungo hai vya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, Wakristo wanaweza kujifunza mengi kutokana na historia hii.Waamini watumie fursa mbali mbali kushirikisha furaha ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanaoendelea kuteswa na kunyanyasika, huko Mashariki ya Kati, kamwe wasikate tamaa, bali wakuze ndani mwao, imani na matumaini. Wasafishe na kuimarisha imani, ili waendelee kuwa ni mashahidi amini wa Kristo na Injili yake kwa njia upendo na heshima kwa wengine.

Sherehe za Ubatizo wa Bwana Jumapili iliyopita anasema Baba Mtakatifu, ilikuwa ni fursa ya kutafakari imani kwa Kristo na Kanisa. Anawataka vijana kugundua kila siku ya maisha yao neema zinazobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Wagonjwa wachote neema na baraka kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, ili kukabiliana na matatizo yao kwa imani zaidi. Huu ni mwaliko wa kumwilisha ahadi za Ubatizo katika hija ya maisha ya kila siku.







All the contents on this site are copyrighted ©.