Dumisheni tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa
Askofu Malcolm McMahon wa Jimbo Katoliki la Nottingham, Uingereza katika barua yake
ya kichungaji wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria
na Yosefu anasema, changamoto za kuishi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu
Mafundisho ya Kanisa zinapata chimbuko lake kwa Kristo mwenyewe na kwamba, hii ni
dhamana nyeti.
Katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, familia nyingi zinakabiliana
na magumu hasa katika mchakato wa kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha ya ndoa
na familia. Kanisa lina matumaini makubwa katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
maalum kwa ajili ya Familia, ili kuonesha ni kwa jinsi gani Kanisa linatoa kipaumbele
cha pekee kwa maisha ya ndoa na familia katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa
na Jamii kwa ujumla.
Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wanandoa na familia
kujikita katika sala, kwani familia inayosali, itaweza kudumu na kukabiliana na changamoto
za maisha kwa pamoja, bila ya kuteteleka, kwani sala ni uti wa mgongo wa maisha ya
ndoa na familia. Familia zijenge na kudumisha ari na moyo wa Sala na Ibada: kwa kusali
Rozari Takatifu mara kwa mara; kwa kusoma na kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja kama
Familia.
Mababa wa Kanisa tangu mwanzo wametambua na kuthamini maisha ya ndoa
na familia katika maisha na utume wa Kanisa, ndiyo maana Papa Leo wa kumi na tatu
akatangaza Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia kwa Kanisa zima.
Askofu McmMahon
anasema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano,
ndoa na familia zinakabiliana na changamoto nyingi za maisha, lakini hakuna haja ya
kukata wala kukatishwa tamaa kwani Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inapaswa
kuwa ni mfano na kielelezo cha kuigwa na waamini wote.
Familia iwe ni mahali
ambapo wanafamilia na majirani wanaonjeshana tone la upendo na msamaha. Hapa ni mahali
pa kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Familia iwe ni
chemchemi ya upendo na ukarimu kwa watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali
ya maisha kama vile wakimbizi, wahamiaji na wote waliokumbwa na maafa asilia sehemu
mbali mbali za dunia.
Familia iwe ni mahali pa kulinda, kuendeleza na kurithisha
tunu bora za maisha ya ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, ndoa ni muungano thabiti
kati ya Bwana na Bibi na wala si jambo la mpito! Huu ndio uelewa kadiri ya mpango
wa uumbaji na ukombozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu na kwamba,
ndoa ni kielelezo cha upendo wa juu kabisa kwa Kristo na Kanisa lake!
Licha
ya magumu na changamoto za maisha ya ndoa na familia, lakini bado kuna wazazi na walezi
wanaowapenda na kuwathamini watoto wao katika malezi na makuzi; kwani wanatambua kwamba,
familia ni kitovu cha kurithisha imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo.
Askofu
Malcolm McMahon wa Jimbo Katoliki la Nottingham katika barua yake ya kichungaji anasema,
kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameziona changamoto za maisha ya ndoa na familia,
ndiyo maana ameitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Ndoa, itakayoadhimishwa
mjini Vatican Mwezi Oktoba, 2014.
Maswali dodoso yaliyotolewa na Baraza la
Kipapa kwa ajili ya Familia yanalenga kujenga na kuimarisha majadiliano kati ya Kanisa
la Waamini katika masuala ya ndoa na familia, ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu
mkakati wa kichungaji utakaosaidia familia kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani
ya Kanisa.