Angola kwa mara ya kwanza inatarajia kuadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa 2015
Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, linatarajia kunako Mwaka 2015 kuadhimisha kwa
mara ya kwanza Siku ya Vijana Kitaifa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, vijana kutoka
nchini Angola wanapewa nafasi ya kuweza kushirikisha karama na vipaji vyao kwa ajili
ya ujenzi, ustawi na maendeleo ya Kanisa na Taifa katika ujumla wake. Hayo yamejadiliwa
hivi karibuni katika Bunge la Vijana wa Angola.
Askofu Zeferino
Martins, Mwenyekiti wa Tume ya Vijana ya Baraza la Maaskofu Katoliki Angola anasema,
vijana wengi nchini humo wanakabiliwa na tatizo la ulevi wa kupindukia, hali ambayo
inabomoa misingi bora ya maisha ya kikristo na kiutu, kiasi hata cha kudhohofisha
maisha ya ndoa na familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Angola linasema, kuna haja
kwa wadau mbali mbali kuwekeza katika majiundo makini ya vijana, ili kudhibiti tabia
ya ulevi ambayo inawatumbukiza vijana hata katika majanga mengine ya maisha.
Maaskofu
wanasema, umefika wakati kwa Angola kutoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume
wa Familia. Changamoto hii inakwenda sanjari na maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi
maalum ya Maaskofu kuhusu Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.