Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini ndiye
aliyeongoza Warsha ya Siku moja iliyokuwa imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Sayansi
Jamii kuhusu hali tete nchini Syria kutokana na maelfu ya watu wanaoendelea kupoteza
maisha yao na wengine kulazimika kuyakimbia makazi yao.
Wajumbe wa warsha
hii, wanasema, kuna haja kwa wadau mbali mbali kuanzisha mchakato wa upatanisho na
ujenzi mpya wa Syria unaosimikwa katika haki na amani. Wahusika wakuu katika mgogoro
huu waoneshe utashi wa kisiasa wa kutaka kumaliza mgogoro huu kwa njia ya amani. Nchi
za nje ambazo zimekuwa zikiendelea kufanya biashara ya silaha nchini Syria zinapaswa
kusitisha mara moja, ili kuokoa maisha ya watu na kama sehemu ya kwanza ya mchakato
wa upatanisho.
Baada ya kusitisha mapigano, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuanza juhudi za ujenzi mpya wa Syria kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kupata
mahitaji msingi, tayari kushiriki katika ujenzi wa nchi yao. Ujenzi huu unaweza kuanza
tu, ikiwa kama masuala ya kisiasa na kijamii yatakuwa yamepatia ufumbuzi wa kudumu.
Vijana na maskini wapewe kipaumbele cha kwanza, ili kuwawezesha kupata ajira sanjari
na kuchangia kwa hali na mali katika ujenzi mpya wa Syria.
Wananchi wa Syria
hawana budi kuanza kujielekeza wenyewe katika majadiliano ya kina yanayosimikwa katika
ukweli na uwazi; upendo na mshikamano wa kitaifa, ili kuendeleza dhana ya upatanisho
wa kitaifa unaopania pamoja na mambo mengine kufukia chuki na uhasama uliojitokeza
katika siku za hivi karibuni, ili watu waanze tena kuaminiana na kusaidiana kwa hali
na mali kama ndugu.
Jumuiya ya Kimataifa inatambua kwamba, ukosefu wa amani
na utulivu nchini Syria unaweza kusababisha athari kubwa katika eneo la Mashariki
ya Kati. Kuna mataifa makubwa ambayo yanaendelea kujiimarisha huko Syria kwa sababu
za kiuchumi. Amani na usalama ni mambo yanayowezekana nchini Syria kwani historia
inaonesha kwamba, wananchi wa Syria kwa miaka mingi waliweza kuishi kwa amani na utulivu
na kwa sasa wanaweza pia kuanza kufanya hivyo.
Wajumbe wa Warsha kwa ajili
ya Syria wanasema, Awamu ya Pili ya Mkutano wa Syria huko Geneva ujitahidi kuwashirikisha
wadau wote ndani na nje ya Syria yenyewe kwa kuzingatia pia makubaliano yalihyofikiwa
kati ya Irani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kuhusiana
na masuala ya Kinyuklia, ili kujenga na kuimarisha hali ya kuaminiana na kushirikiana,
ili hatimaye, kupata amani ya kudumu nchini Syria. Majadiliano kati ya Israeli na
Palestina hayana budi kusonga mbele kwa kusaidiwa na Marekani ambayo imekuwa ni mshiriki
mkubwa.
Wajumbe wa warsha hii iliyofanyika katika faragha wanasema, amani ya
kudumu inasimikwa katika msingi wa utashi wa kisiasa wa kusitisha mapigano; kuanza
majadiliano ya kweli kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali. Awamu ya Pili ya mkutano
wa Syria huko Geneva uwe ni msingi wa amani ya kudumu na mwanzo wa mabadiliko ya kisiasa
na kijamii nchini Syria. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukumbusha kwamba, vita
kamwe haiwezi kuwa ni njia ya amani. Wananchi washinde ubinafsi kwa kuongozwa na dhamiri
nyofu kutafuta mafao ya wengi kwa njia ya majadiliano na upatanisho; ili kudumisha
amani na maridhiano.