2014-01-14 10:51:56

Simameni kidete kujenga nchi katika misingi ya haki, amani na upatanisho!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya Kati, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati katika ujenzi wa nchi yao, huku wakithamini mchango unaotolewa na Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Hivi karibuni Mama Kanisa ameadhimisha Sherehe za kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mfalme wa Amani aliyekuja kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na woga.

Inasikitisha kuona kwamba, wananchi wengi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaelemewa sana woga na majonzi ambayo kwa sasa yamekuwa ni chakula chao ya kila siku. Wakati dunia ilikuwa inasherehekea na kufurahia kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kwa bahati mbaya, wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati walikuwa wanajikita katika mauaji ya ndugu na jirani zao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya Kati linasikitika kwa machafuko ya kisiasa na kijamii yalivyoruga amani, upendo na mshikamano hata kwa nchi jirani kwa kulazimika kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama wa maisha yao.

Maaskofu wanasema hawaungi mkono dhana ya kutaka kuigawa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa misingi ya udini na ukabila, badala yake, wananchi washikamane katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao ambao kwa sasa inahitaji sera na mikakati makini ili kuweza kuwajengea wananchi matumaini mapya yanayosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na upatanisho wa kitaifa.

Wananchi wajiandae kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ili kufupisha utawala wa kipindi cha mpito. Kuna haja ya kuunda Tume ya Kimataifa itakayochunguza kwa dhati ukiukwaji wa haki msingi za binadamu nchini humo. Wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanyang'anywe ili kulinda na kudumisha amani na utulivu.

Watu wajikite katika majadiliano ya kisiasa, kidini na kiekumene, ili kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya Kati linawashukuru wahisani na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwasaidia wananchi wao katika ujenzi mpya wa Afrika ya Kati.







All the contents on this site are copyrighted ©.