2014-01-14 09:08:28

Mshikamano, umoja na udugu ni mambo yanayopania kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu katika misingi ya haki na amani!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva anasema kwamba, Vatican itaendelea kuhamasisha utamaduni wa kujadli, kuthamini na kulinda utu na heshima ya binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo na hali ya kutojali wala kuthamini watu wengine katika shida na mahangaiko yao.

Kwa njia hii, Jamii itaweza kuanza mchakato wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko. Umefika wakati wa kuchuchumilia Injili ya Uhai na kuachana kabisa na matumizi ya silaha kama njia ya kutatua mataizo ya kisiasa na kijamii yanayozikabili nchi nyingi duniani kama inavyojitokeza huko Syria.

Vyombo vya upashanaji habari visaidie mchakato wa kuelimisha Jamii umuhimu wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kwa hali na mali. Tofauti za imani na dini; rangi na kabila zisiwe ni chanzo cha vita na kinzani za kijamii; watu watambue kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; tofauti zao ni utajiri unaopaswa kuthaminiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Udugu ni msingi na njia ya kujenga na kudumisha amani kwa kushinda kishawishi cha migawanyiko ya Kijamii, Ubinafsi, uchu na uroho wa mali na madaraka. Ikumbukwe kwamba, vita itaendelea kuwa ni chanzo kikuu cha uvunjifu wa misingi ya haki na kwamba, vita inasababisha mateso na mahangaiko ya kwa watu wasiokuwa na hatia.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anabainisha kwamba, mchango wa wawakilishi wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa na Mashirika mbali mbali mbali ya Kimataifa unapania kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kujenga na kuimarisha ushirikiano na mshikamano wa kidugu unaosimikwa katika kanuni ya auni, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema jitihada za kutafuta amani huko Mashariki ni za siku nyingi zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa. Vita inayoendelea nchini Syria ni matokeo ya kinzani za kivita nchini Iraq, hali ambayo inasababisha mateso na usumbufu mkubwa kwa mamillioni ya watu wasiokuwa na hatia huko Syria.

Jambo la msingi kwa sasa, Jumuiya ya Kimataifa inataka wahusika wa mgogoro wa kivita nchini Syria kusimamisha mapigano ambayo yanaendelea kusababisha majanga kwa wananchi wengi na kuanza majadiliano, ili kuweza kupata suluhu na amani ya kudumu. Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa kwa Awamu ya Pili ya Mkutano kwa ajili ya Syria huko Geneva.







All the contents on this site are copyrighted ©.