Kinzani za kijeshi nchini Msumbiji zinaweza kusababisha maafa makubwa!
Wasi wasi wa kuvunjika kwa amani unaendelea kuongezeka nchini Msumbiji kutokana na
kinzani zinazojitokeza kati ya Jeshi la Serikali linaloongozwa na Chama cha FRELIMO
na Jeshi la Waasi kutoka Chama cha upinzani cha RENAMO. Mapigano ya hivi karibuni
kati ya Jeshi la Serikali na Renamo, wilayani Homoime, Jimbo la Inhambane yamepelekea
watu kadhaa kupoteza maisha.
Mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Jeshi
la Serikali ya Msumbiji kwenye Makao makuu ya RENAMO, mwanzoni mwa Mwezi Oktoba, 2013
yalisababisha uhusiano kati ya RENAMO na FRELIMO kusuasua kwa kiasi kikubwa na hapo
ukawa ni mwanzo wa kutoweka kwa amani nchini Msumbiji. Inasikitisha kuona kwamba,
vita ya wenyewe kwa wenye iliyodumu nchini Msumbiji tangu Mwaka 1975 hadi Mwaka 1992
inataka kuzuka tena.
RENAMO inataka kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi nchini
Msumbiji pamoja na kuwa na usawa katika ugavi na matumizi ya rasilimali za nchi kuliko
hali ilivyo kwa sasa kwani inasemekana kwamba, wanaofaidi zaidi ni viongozi wa Serikali
iliyoko madarakani wanaotumia nyadhifa zao kuwanyanyasa viongozi wa vyama vya upinzani.