Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua Makardinali wateule kwa kuwahakikishia
uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, baada ya kuteuliwa kuwa washiriki na wasaidizi
wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawaalika kwa namna ya pekee Makardinali
kujivika karama na matamanio ya Yesu Kristo, ili waweze kushiriki kikamilifu katika
kumsaidia Baba Mtakatifu kutekeleza wajibu na dhamana yake kwa Kanisa la Kiulimwengu.
Baba
Mtakatifu anawakumbusha Makardinali wapya kwamba, kwa kuteuliwa kwao kuwa Makardinali
si kwamba, wamepandishwa cheo na kupewa heshima, bali ni huduma inayowataka kuwa na
mwelekeo na moyo mpana zaidi. Ni changamoto ya kuwa na mwono mpana na kupenda wote,
kwa njia ya unyenyekevu kwa kujifanya kuwa mtumishi wa wote.
Baba Mtakatifu
anawaalika kupokea uteuzi wake kama jambo la kawaida kwa moyo wa unyenyekevu. Wajitahidi
kuonesha furaha yao mintarafu moyo wa kiinjili kwa kujinyima, kiasi na kuzingatia
fadhila ya ufukara.
Baba Mtakatifu anawakaribisha kwa mikono miwili hapo tarehe
20 Februari 2014, watakapoanza siku mbili za tafakari ya kina kuhusu Familia. Baba
Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa kujiweka mbele yao wakati wowote watakapomhitaji
na kwamba, waendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya Sala.