2014-01-14 12:00:53

Acheni unafiki ambao ni kikwazo kikubwa cha ushuhuda wa imani!


Wakristo wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo adili kwa kuachana na unafiki na makwazo yanayowafanya baadhi ya waamini kulikimbia Kanisa. Yesu alikuwa anafundisha kama kiongozi aliyekuwa na mamlaka na wala si kama walivyofanya Mafarisayo na Waandishi waliokuwa wanawabebesha wengine mizigo mizito!

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo Jumanne, tarehe 14 Januari 2014, wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha mjini Vatican. Anasema, imani inapaswa kutangazwa, kufundishwa na kushuhudiwa kwa njia ya matendo na kwamba, imani ni hazina kubwa ambayo inapaswa kulindwa na kutetewa kwa njia ya maisha. Ni mwaliko wa kusali bila kuchoka kama ambayo Hana anavyosimuliwa kwenye Kitabu cha kwanza cha Samweli.

Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya viongozi wa Kanisa wanashindwa kutekeleza wajibu wao barabara na badala yake wanaelemewa mno na uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo yanawakwaza waamini walei na kumsaliti Yesu anayewaita ili kushiriki katika dhamana ya Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Viongozi na waamini wala na watoa rushwa ni mzigo mkubwa kwa Kanisa.

Yesu aliwavuta wengi na wakashangazwa mno na mahubiri yake kutokana na utakatifu wa maisha uliokuwa unabubujika kutoka katika undani wa maisha yake. Aliwapatia watu chakula cha maisha ya kiroho, akaganja njaa yao kwa kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwa kuwasamehe pia dhambi zao. Alionesha mshikamano wa upendo na wadhambi, ili waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Yesu alijitahidi kugusa mioyo ya watu ili awavute kumwelekea Mwenyezi Mungu, awagange na kuwaponya kutoka katika undani wa maisha yao. Ushuhuda wa maisha ya Yesu, kilikuwa ni kielelezo cha Mafundisho Mapya; Ukweli na uwazi wa Kiinjili.

Baba Mtakatifu anawaalika Viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao, kusoma na kulitafakari kwa kina Neno la Mungu, ili liweze kuwasaidia kuwa wakweli na waaminifu kwa Kristo na Injili yake. Wasielemewe na mmong'onyoko wa kimaadili na kuwa kikwazo kwa wengine, bali wajitahidi kumfuata na kuiga mfano wa Yesu Kristo mchungaji mwema.

Viongozi wa Kanisa wajitahidi kuwatafuta wale waliopotea; kuwaganga waliojeruhiwa na kuwapenda wanaotembea na kuogelea katika upweke, huzuni na hali ya kukata tamaa ya maisha. Kimsingi, kila mtu aonjeshwe upendo na huruma ya Mungu, kielelezo makini cha Mafundisho Mapya yanayotolewa na Kristo mwenyewe.







All the contents on this site are copyrighted ©.