Mwanaharakati na mtetezi wa walemavu akutana na Papa Francisko
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 11 Januari 2014 alikutana na kuzungumza
na Mheshimiwa Ileana Argentin, mlemavu na mwanaharakati anayefahamika sana kwa kutetea
haki za walemavu Jijini Roma na katika Bunge la Italia.
Mheshimiwa Ileana
alikuwa amemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko, kumwomba ili aweze kukutana naye
ili kumshirikisha kuhusu hali ya walemavu na baada ya kitambo kifupi, Baba Mtakatifu
aliweza kumjibu na kumpatia nafasi ya kukutana naye Jumamosi iliyopita, mazungumzo
ambayo yamedumu kwa takribani nusu saa.
Akielelezea kuhusu mkutano huu, Padre
Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Mheshimiwa Ileana amemwomba
Baba Mtakatifu asaidie harakati za kuwawezesha wazazi wenye watoto wenye ulemavu ili
waweze kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa heshima na hali ya kiutu, kuliko hali
ilivyo kwa sasa. Wasi wasi ni kuhusu hali ya watoto walemavu pale wanapofiwa na wazazi
wao, wanajikuta katika mazingira magumu zaidi kwani hata wakati mwingine wanashindwa
kupata huduma kutoka kwa ndugu zao wa karibu.
Mheshimiwa Ileana amegusia pia
vikwazo wanavyokumbana navyo walemavu kutokana na miundo mbinu mingi ambayo bado haijatoa
kipaumbele kwa watu wenye ulemavu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake,
ameguswa na mchango wa Ileana Argentin, amemhakikishia uwepo wake wa karibu ili kuwatia
moyo wanaharakati wanaosimama kidete kulinda na kutetea haki za walemavu, ili Jamii
iweze kujihusisha zaidi kuyatafutia ufumbuzi matatizo wanayokumbana nayo!