2014-01-11 09:30:57

Upendo kwa Kristo na Kanisa lake ni hamasa kubwa kwa Kikosi cha waamini walei wanaojitolea bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma mjini Vatican!


Kwa Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, Mama Kanisa anafunga rasmi kipindi cha Noeli, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kutolea ushuhuda kwa Yesu Kristo kwa njia ya imani tendaji inayojidhihirisha kwa namna ya pekee kwa njia ya unyenyekevu, moyo na ari ya huduma pasi na makuu; mambo ambayo Yesu mwenyewe amewafundisha wafuasi wake kwa njia ya mfano wa maisha yake!

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo, Ijumaa, tarehe 10 Januari 2014 alipokutana na Kikosi cha Waamini Walei wanaosaidia shughuli mbli mbali mjini Vatican. Amewashauri kumuiga Kristo, Mwana wa Mungu katika utekelezaji wa majukumu yao kwani Yesu alikuja ulimwenguni si kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumikia na kwa njia hii kazi inakuwa ni sehemu ya utume wa kuwamegea wengine Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Jambo hili linawezekana ikiwa kama mwamini atajikita katika maisha ya sala kama njia ya majadiliano na Mwenyezi Mungu. Waamini wajifunze moyo wa ukarimu na majitoleo kutoka kwa Kristo mwenyewe. Kikosi hiki ni cha watu ambao wamehamasika zaidi kulipenda Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro; kiasi kwamba: fadhila ya ukarimu, uvumilivu, subira na amani ya ndani ni tiketi muhimu sana kwa watu mbali mbali wanaotembelea mjini Vatican ili kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu amewashukuru kwa uwepo na huduma yao makini kwa ajili ya Kanisa. Anawashukuru kwa jinsi wanavyomsaidia kukutana na kuzungumza na watu si tu katika wingi wao, bali hata mtu mmoja mmoja, hasa watoto wanaoletwa na Mama zao kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ili kupata baraka kutoka kwake. Baba Mtakatifu amewataka wafanyakazi hao kuwa mstari wa mbele kulinda na kuwatunza watoto wao, kwa kuwaonesha na kuwamegea upendo wa dhati.

Habari zaidi kutoka mjini Vatican zinasema kwamba, kabla ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, Baba Mtakatifu alifanya ziara ya ghafla kwa wafanyakazi hawa, katika eneo lao la kazi, wanapojiandaa kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma kwenye matukio mbali mbali mjini Vatican na kuzungumza nao kwa kitambo. Wafanyakazi hawa walishika tamaa kwa mshangao na baada ya kitambo kidogo, wote wakajawa na furaha na moyo wa shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko anayeonekana kuwajali zaidi wanyonge.

Waamini hao walei wanasema, kwao ni neema, baraka na fursa ya pekee kabisa kuweza kutoa huduma yao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro hasa pale anapotembelewa na: Wakuu wa nchi, Mabalozi na watu mashuhuri. Kutokana na huduma hii, wanajikuta hata wao kuwa ni sehemu ya Familia ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa huduma na utume wao kwa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.